- Kukutana na makocha kujadili
- Tenga akerwa na mwanamke wa Taita
Na Asha Kigundula
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakutana na makocha wa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara na makocha wa timu za Taifa kuangalia kwa kina tatizo la wachezaji kutokuwa na nguvu baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema ameona kuna umuhimu mkubwa wa kujua nini tatizo kwa timu za Taifa zinapocheza dakika 45 na hata ligi kwa ujumla.
Tenga alisema amekaa na Kamati ya Ufundi ya TFF na kuangalia nini wafanye na kuamua ni bora wawaite makocha hao na kuzungumzia kwa pamoja suala hilo.
Alisema hata kufanya vibaya kwa timu yaTaifa ya Kilimanjaro Stars si ubovu wakikosi au uwezo wa makocha tatizo ni kutokuwa na nguvu baada ya dakika 45 za mwanzo.
Tenga alisema makocha Jamhuri Kihwelo na Charles Mkwasa ni makocha wazuri sana ambao wana uzoefu na timu ya taifa, tatizo kubwa ni wachezaji kuishiwa nguvu mapema.
Alisema tatizo la nguvu ni la muda mrefu limekuwa likionekana katika mechi nyingi na si katika michuano ya Chalenji pekee ambayo imemalizika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Tenga alisema hata suala la kuweka kambi kwa muda wa wiki tatu au mwezi siku hizi hakuna hivyo kufanya kwao vibaya ni kutokana na nguvu na si kingine.
Alisema hata timu za Kenya, Uganda na Sudan zilikutania Uwanja wa ndege wakati zinakuja nchini kushiriki lakini zilifanya vizuri kutokana na wachezaji kuwa na nguvu nyingi.
Tenga alisema kutokana na kufanya vibaya huko kila siku makocha wataonekana hawana uwezo, wakati kumbe ni nguvu na si jambo jingine.
"Ukweli ni kwamba kuna umuhimu mkubwa wa sisi (TFF) kukutana na makocha wa timu za Taifa na hata wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu kwa ajili ya kuangalia tatizo hili la nguvu kwa wachezaji wetu baada ya kipindi cha kwanza tu, tusipofanya hivi, kila siku tutakuwa tunafukuza makocha kumbe tatizo ni hili," alisema Tenga.
Pia, Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kuacha kuwazomea wachezaji wao wakiwa katika mechi za taifa kwa ajili ya kuwajengea morali badala ya kuwavunja moyo.
Alisema si kweli kama kila siku timu hizo za Taifa huwa zinafanya vibaya, kikubwa ni kuwashangilia waweze kujiona kuna watu wapo karibu yao wakiwasapoti.
Wakati huohuo, Tenga amesikitishwa na kushangazwa na taarifa za mchezaji wa Yanga na taifa Stars, Geofrey Taifa kuingiza mwanamke katika kambi ya timu ya taifa iliyokuwa kwenye michuano ya Kombe la Chalenji.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo aliuliza makocha wa timu hiyo, Julio na Mkwasa, ambao nao walimjibu kwa mshangao wa kutojua jambo hilo limetokeaje na kwa nini.
"Wakati wapo Sinza, kila siku tulikuwa tukipata taarifa za wachezaji wa Stars, ndio sababu ya kufanya mabadiliko haya ambayo nayo ndiyo kama hivi, hata mimi nilishangaa kusikia mchezaji ameingiza binti kambini, ni kitendo cha ajabu sana," alisema Tenga.
Aidha, rais huyo amesema atakutana na makocha wa timu hizo kupanga adhabu kali katika makosa kama hayo yanapotokea ili kuondoa aibu kwa taifa.
Saturday, December 17, 2011
New
Uchovu wa wachezaji waishitua TFF
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment