FATUMA YASSIN: - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, February 7, 2012

FATUMA YASSIN:

FATUMA YASSIN:
Mkali wa sauti anayeibuka kivyake
- Aliing'arisha Segere kwa 'Usia wa Mama'
- Kwa sasa anakamua na Kings Modern

Na Hamisi Magendela
FATUMA Yassin ni miongoni mwa wanamuziki wa kundi ka Kings Modern Taarab anayefikiria kuachana na fani hiyo kutokana na vikwazo mbalimbali anavyokumbana navyo katika ulingo huo.
Msanii huyo aliyeanzia katika kundi la DDC Kibisa akiwa mwimbaji mwanafunzi, aliweza kushiriki katika nyimbo nyingi akishiriki zaidi katika sehemu ya kiitikio.
"Tangu nijiunge katika katika kundi la DDC Kibisa mwaka 1999, licha ya kuwa na sauti nzuri ya kumtoa nyoka pangoni, lakini sijapata bahati ya kubeba wimbo, kitu ambacho kinanikatisha tamaa kuendelea na fani hiyo," anaanza kwa kusema Fatuma.
Mwanamama huyo aliyezaliwa Julai 14, 1977 katika Hospitali ya Ocean Road, anasema aliamua kuingia katika fani hiyo baada ya kuvutiwa na wanasanii waliokuwa wakifanya vizuri kwa wakati huo akiwemo Nasmah Hamisi 'Kidogo' (marehemu), sanjari na Hadija Kopa.
Anasema alidumu katika kundi hilo kwa miaka mitatu, baada ya kupata ujauzito wa mtoto wa kwanza na akaendelea na muziki mwaka 2005 katika kundi lingine la Segere Wazazi Cutural na kushiriki kuimba katika kibao kilichofanya vizuri kinachojulikana na 'Usia wa Mama'.
Msanii huyo anaweka wazi kuwa mwaka 2008 alilikacha kundi hilo na kuhamia kundi jipya lililloanzishwa kipindi hicho la Kings Modern linaloongozwa na Hamisi Majaliwa akisaidiana na Nassor Hamisi 'Kijoka'.
Baada ya kufika katika kundi hilo alipokelewa kwa mikono miwili na kupewa ushirikiano wa kutosha, hali inayompa matumaini ya kufanya vizuri katika ulingo huo.
"Ni kweli hapa nilipo napewa ushirikiano wa kutosha hali inayonipa matumaini ya kufanya vizuri na kukonga nyoyo za mashabiki katika maonesho mbalimbali tofauti na mwanzo," anasema.
Alisema katika kuleta ufanisi katika tasnia ya muziki huo ni vizuri  wasanii wakazingatia nidhamu kitu kitakacholeta maendeleo ya fani hiyo.
Alisema nidhamu ni kitu muhimu katika kazi ya aina yoyote na kuamini kuwa yeye binafsi ndiyo iliyomfikisha hapo alipo na kuwataka wasanii wengine kuacha dharau.
Pia, anasema katika maisha yake ya sanaa na pamoja na nyumbani, anachukia kuona baadhi ya watu wakiendekeza majungu ambayo mwisho wake ni mbaya.
"Riziki siku zote hupangwa na Mungu na ninachowaomba wasanii kwa ujumla kuachana na majungu ambayo yatawapotezea muda," anaonya Fatuma.
Nyota huyo alihitimu elimu ya msingi katika shule ya Uhuru Mchanganyiko mwaka 1987, anasema kuwa malengo yake ya siku chache zijazo ni kufyatua albamu yake mwenye.
Anasema amefikiria kufanya hivyo ili kuonesha kiwango chake katika medani ya muziki huo na anaamini kuwa atafanya vyema kutokana na ushirikiano anaotarajia kupata kutoka kwa viongozi wake.
"Kila kitu kinakwenda kwa ushikiano na hata hapa nilipo nisingefika ila kwa ushirikiano wa watu mbalimbali akiwemo Kijoka na wengineo ambao waliweza kunisaidia kwa moyo wao wote, anazidi kufunguka.
Anasema kwa kudhihirisha hilo, kwa sasa anaufanyia mazoezi wimbo mpya unaofahamika kwa jina la 'Binadamu Hafadhiliki' uliotungwa na Mkurugenzi Msaidizi wa kundi hilo.
Mwimbaji huyo mwenye watoto watatu, Ali Salum (14), Nasri Salum (12), Marik Salum 'Yuda' (7) anasema kibao hicho kutokana na utunzi wake kuwa makini anaamini utakuwa bora na kuteka mashabiki mbalimbali wa kundi hilo.
Anasema kwa sasa anajipanga kuachia albamu yake mwenyewe kwa lengo la kudhihirisha uwezo wake pindi mambo kadhaa yatakapokamilika.
Anabaisha kuwa kwa sasa yuko 'singo' baada ya kuachana na mzazi mwenzake miaka kadhaa iliyopita kwa sababu mbalimbali ambazo hakuziweka wazi, lakini bado anaweza kumudu kufanya kazi na kuilea familia yake akiwa peke yake.
Fatuma Yassin msanii wa taarabu wa kundi la kings Modern

No comments:

Post a Comment