- MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, February 7, 2012

Real Promise ya Rose Ndauka balaa
Na Hamisi Magendela
KAMPUNI ya Faisal Production ikiwa miongoni mwa taasisi chache zenye lengo maalum la kuhakikisha fani ya filamu inastawi na kupata maendeleo nchini, imeandaa kazi mpya inayokwenda kwa jina la Real Promise.
Katika filamu hiyo ambayo tayari imeanza kuwa gumzo la jiji, waigizaji nyota kama Mohammed Mwikongi 'Frank', Rose Ndauka, Bambucha na Rania wameshiriki na kufanya makubwa ambayo yatamfanya mtazamaji kutopata muda wa kufanya shughuli nyingine.
Kwa mujibu wa msemaji wa kampuni hiyo, Feisal, filamu hiyo kwa sasa iko katika hatua ya uhariri, akisisitiza kutoa tungo bora kabisa sambamba na kuchezwa vizuri na wahusika.

Real Promise inazungumzia mikasa ya mapenzi na hatua mbalimbali za kukabiliana nayo ikizingatiwa kuwa mapenzi ni sehemu kubwa ya maisha ya kila siku ya binadamu.
Rose, ambaye ameng'ara katika filamu nyingi hapa nchini, amefanya makubwa katika kazi hiyo inayotarajiwa kutoka wakati wowote mwezi huu.

Kijacho cha Sajuki kina mambo
Na Hamisi Magendela
HII kali! Filamu nyingine kali ambayo inaingia sokoni hivi karibuni kwa jina la Kijacho inataka kufukua mapya yaliyo nyuma ya pazia.
Kwa mujibu wa waandaaji wa filamu hii, ambayo imeongozwa na mkali wa sanaa hiyo hapa nchini, Juma Kilowoko 'Sajuki', itakuwa na mambo mengi ya kufumbua macho watu.
Sajuki alisema kazi kubwa iliyofanywa na wasanii watakaoonekana katika filamu hii ni kuonesha jinsi ujauzito unavyoweza kubeba siri kubwa kwa jamii.
"Kuna mambo mengi ambayo yanaweza kukufanya ukashangaa ndani ya familia yako, lakini tunaamini kuwa mtoto mpya katika familia huongeza upendo kwa wazazi wake," alisema Sajuki.
Katika kufichua kinachoonekana ndani ya Kijacho, Sajuki amesimama sawasawa na mkewe, Wastara Juma na Salim Ahmed.


Daraja la Kwanza kutumia viwanja 7 leo
Na Asha Kigundula
LIGI Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kutimua vumbi leo kwa timu 14 zitakuwa kwenye viwanja saba katika hatua ya makundi.

Timu ya Transit Camp na Mgambo Shooting zitachuana kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mechi pekee ya Kundi A itakayochezeshwa na mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam.

Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya kutakuwa na mchezo kati ya Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Small Kids.

Timu ya JKT Mlale itaoneshana kazi na Mbeya City kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Na Polisi Iringa itacheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.

Mechi za Kundi C zitakuwa kati ya Polisi Morogoro na Morani FC itakayopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, AFC na Rhino washuka kwenye Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha na Polisi Tabora itakuwa mwenyeji wa 94 KJ kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

TFF yatuma Ombi la Yanga CAF
Na Asha Kigundula
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) jana limetuma maombi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), likitaka wacheze mechi moja tu ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri ili
kujiepusha na machafuku yalijitokeza nchini humo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa wameshatuma maombi hayo ambapo sasa wanasubiri majibu kutoka CAF.
Wambura alisema kuwa Yanga iliwapelekea maombi yao juzi, ambapo jana walikuwa na kazi kubwa moja ya kuhakikisha kuwa yanawafikia CAF kwa wakati.
Alisema kuwa, hata hivyo, suala hilo lipo zaidi kwa timu ya Zamalek, ambayo ndiyo inayocheza na Yanga kama itakubali au kutafuta nchi nyingine.
"Sasa tunasubiri CAF kama watakubali au la, lakini kikubwa ni kwamba wenye uamuzi wa mwisho ni Zamalek," alisema Wambura.
Ombi hilo lilitolewa na viongozi wa Yanga wakihofia hali ya usalama kuwa ndogo nchini Misri katika siku za hivi karibuni, na kuona ni bora mechi ikachezwa moja.
Walisema wao wapo tayari kucheza mechi moja ambayo mshindi wake atasonga mbele katika hatua inayofuata.
Wanaowania uongozi DRFA wafikia 11
Na Asmah Mokiwa
WADAU wa soka wa Mkoa wa Dar es Salaam wamezidi kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi tofauti za uongozi katika chama cha mkoa huo (DRFA).
Wadau hao waliojitokeza ni pamoja na Mohammed Bhinda, aliyechukua fomu kwa ajili ya kutetea kiti chake cha Mwakilishi wa Klabu na Hamisi Kisiwa, alichukua fomu ya kuwania kiti cha Umakamu Mwenyekiti.
Kutokana na hilo, idadi ya wagombea sasa imefikia 11, ambao tayari wameshachukua fomu kuwania nafasi tofauti katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi 18 mwaka huu, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Harudiki Kabunju, alisema leo ndio mwisho wa kuchukua fomu hizo, hivyo wadau wengine watumie nafasi hiyo kama wanataka kugombea.
Wagombea wengine waliochukua fomu hizo ni pamoja na Muhsin Balhabou, anayewania Ujumbe wa kuiwakilisha Dar es Salaam katika Mkutano Mkuu wa Shirikishi la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ali Obe (Mweka Hazina), Salum Kadudi na Kanuti Daudi (Ujumbe wa Kamati ya Utendaji).
Wengine ni Sanifu Kondo (Katibu Mkuu), Abeid Mziba (Ujumbe), Hamisi Mkwama, Bungu Tambaza (Ujumbe) na Lameck Nyambaya, anayewania nafasi ya Mjumbe anayewakilisha klabu.
Alisema kuwa zoezi hilo la utoaji fomu litamalizika leo na kuwataka wote wenye nia ya kugombea nafasi hizo za uongozi kujitokeza mapema.
Aliongeza kuwa kamati hiyo ya uchaguzi inayoongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), Muhidin Ndolanga, itaendesha zoezi la usaili wa ifikapo Februari 14.
Alisema pia, Februari 15 watatangaza majina ya wagombea wote waliopitishwa kuwania nafasi ambazo watakuwa wameziomba wenye na Februari 16 na 17 ni siku za kupokea mapingamizi.
Simba yaitia nyodo Villa Squad
Na Asmah Mokiwa
WACHEZAJI wa timu ya soka ya Villa Squad wamesema ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba umemsha ari ya kufanya vyema katika mashindano ya ligi msimu huu.
Villa ilifanikiwa kuisimamisha Simba baada ya kipa wa Wekundu wa Msimbazi, Juma Kaseja kushindwa kuzuia shuti la Nsa Job, lililozaa bao pekee la Villa Squad.
Akizungumza na Jambo Leo Dar es Salaam jana, mshambuliaji wa Villa, Mussa Mohammed, alisema watajitahidi timu hiyo kutoshuka daraja kwa kuendeleza ushindi.
Alisema licha ya kufungwa mechi nyingi na kumaliza vibaya mzunguko wa kwanza wa ligi, bado wana nafasi ya kufanya vizuri katika mechi zilizobaki za Ligi Kuu.
Mohammed alisema kutokana na kufanya vyema katika mechi hiyo, wamepanga kuendeleza mashambulizi kwa timu yoyote watakayokutananayo ili kujitoa mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo.
Alisema wamepanga kufuta historia ya timu hiyo kwamba ni timu inayoshuka daraja kila inapopanda kushiriki Ligi Kuu kwa kushindwa kuhimili mikiki mikiki yake.
"Tutahakikisha timu yetu haishuki daraja msimu huu, kwani tumeanza vibaya mashindano, tutajitahidi kumaliza ligi kwa kuendelea kubaki na kushiriki ligi ya msimu ujao na si kushuka daraja tena," alisema Mohammed.
Nyota wa Mtibwa aombewa ITC kukipiga Thailand
Na Asha Kigundula
TIMU ya Roiet FC ya Thailand imeomba Hati ya  Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji Michael Victor Mgimwa kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa nchini kwao.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema ombi hilo limetumwa juzi na Chama cha Mpira wa Miguu cha Thailand (FAT).
Wambura alisema maombi hayo yalitumwa kwa TFF ili kupata hati hiyo.

Mgimwa ambaye tayari yuko Thailand ameombewa hati hiyo ili aweze kuichezea timu ya Roiet FC ambayo iko daraja la pili nchini humo.

TFF inafanyia kazi maombi hayo na ITC itatolewa wakati wowote baada ya taratibu husika kukamilika, ikiwemo kuwasiliana na Mtibwa Sugar, ambayo ilikuwa klabu yake ya mwisho hapa nchini.
Coe aleta mpango wa maendeleo ya michezo
Na Hamisi Magendela
MWENYEKITI wa Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya London 2012, Lord Coe, amekutana na wanafunzi wanaoshiriki mpango wa maendeleo  ya michezo kimataifa.
Kiongozi huyo alisema kuwa lengo la kukutana na vijana hao ni kuhamasisha na kuwaunganisha waweze kushiriki katika michezo itakayoboresha maisha yao duniani kote.
Alisema dira ya mpango huo ni kubadilisha maisha ya watoto wakiwemo walemavu walio shuleni na katika jamii kupitia nguvu ya elimu bora ya michezo shirikishi.
Alifafanua kuwa lengo linazingatia katika maeneo manne ambayo ni pamoja na kuwa na walimu wa kutosha wenye mbinu za kufundisha na kuongeza ushiriki wa wanawake.

No comments:

Post a Comment