Na Hamisi Magendela
KOCHA wa mchezo wa tenisi, Salum Mvita amesema sababu kubwa ya kumpeleka mchezaji mmoja katika mashindano ya Kenya Open imetokana na ukosefu wa fedha.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mvita alisema wachezaji waliotakiwa kwenda katika mashindano ni zaidi ya 10 lakini kutokana na ukosefu wa fedha amekwenda mmoja.
"Tatizo ni ukosefu wa fedha kwani hata huyo mmoja amekwenda kwa fedha zake, hivyo ili kuhakikisha timu ya taifa inafikia mafanikio ni vema wafadhiri sanjari na Serikali wakajitokeza kusaidia pindi mashindano kama hayo yanapofanyika," alisema Mvita.
Mvita alimtaja mchezaji anayewakilisha nchi pekee yake kuwa ni Rehema Athumani japo alibainisha kuwa anamatumani kuwa atafanya vema katika mashindano hayo.
"Kiwango chake ni kizuri hivyo ni matumaini yangu kuwa atafanya vema katika mashindamo yaliyoanza Mei 27 mwaka huu na yakitarajiwa kufikia tamati Juni 2, mwaka huu," alisema Mvita.
Pia aliwaomba Watanzania kumwombea dua ili afanikiwe kuiwakilisha nchi vema na kurudi na ushindi licha ya kuwa mmoja katika mashindano hayo.
Wakati timu hiyo ikiwa inawakilishwa na mchezaji mmoja timu ya walemavu imepeleka wachezaji wanne ambao waliondoka juzi na jana walianza kuonesha umahiri wao katika mchezo huo.
No comments:
Post a Comment