* Yataka wadau kujitokeza kuwania uongozi
Na Asha Kigundula
SERIKALI imeridhika na uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa) kuamuru mchakato wa uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza upya na kufanyika kabla ya Oktoba 30, mwaka huu.
Imesema kwa uamuzi huo haki imeonekana kutendeka na mlango kufunguliwa kwa wadau wengine watakaotaka kuwania uongozi kujitokeza.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Amos Makalla, alisema kuwa uamuzi uliotolewa na Fifa umeweza kuondoa hali ya sintofahamu ambayo ilikuwa imetawala kabla na kusababisha uchaguzi kusimamishwa.
![]() |
| Naibu Waziri wa Habari, Michezo na na Utamaduni Amos Makalla. |
Makalla alisema kuwa sasa wanasubiri Kamati ya Tendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) ikutane na kupanga ratiba ya mchakato ikiwemo mkutano wa dharura wa kubadili katiba.
Alisema Fifa imeshawaambia TFF hakuna suala la waraka, Mkutano Mkuu ufanyike kisha ufuatiwe na Mkutano Mkuu wa uchaguzi.
Makalla alisema wakati akizungumzia suala la uchaguzi wa TFF kuna maneno mengi yalisemwa ikiwemo kudai hawakuwa sawa, lakini sasa Fifa wameamuru kile walichoelekeza kabla.
"Nilipoingilia mchakato tff wasiopenda haki walinidhihaki sana nashukuru Fifa wamethibitisha hili ... namshukuru Tenga (Rais wa TFF) kwa ushirikiano aliotupatia Serikali, nawashukuru wadau wa mpira wa miguu kwa ushirikiano na utulivu waliouonesha wakati wa kipindi kigumu cha sintofahamu," alisema Makalla.
Pia Makalla aliwataka wadau wa soka watumie nafasi ya kuanza upya mchakato wa uchaguzi kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali na kuacha malumbano.
"Niwatake wadau wa soka kutumia nafasi hii vizuri wawanie nafasi mbalimbali, tuache malumbano tujenge soka," alisema Makalla.





No comments:
Post a Comment