Na Magreth Magosso, Kigoma
TIMU sita za mpira wa miguu za wanawake Mkoa wa Kigoma zinatarajia kumenyana katika Ligi ya Mkoa ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Taifa .
Akizungumzia suala hilo juzi kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo Kigoma Ujiji , Kocha wa timu ya Kigoma Queens, Madua Kilonzo alisema lengo la kushirikisha timu hizo ni kuibua vipaji vya wasichana kuanzia umri wa miaka 14 hadi 17.
Alisema kuwa kwa kupitia soka, wanawake wanaweza kupata fursa ya kutengeneza ajira kwenye timu maarufu ndani ya nchi na nje ya nchi.
“ Wilaya zitakazoshiriki ni pamoja na Kigoma Ujiji, Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Kakonko na Uvinza kutokana na ushiriki huo wadau wachangamkie fursa ya kuziwezesha timu hizi ili kuwaongezea ujasiri wa kujituma na hatimaye timu iweze kushiriki mashindano ya mpira ambapo ni tija kwa wachezaji na mkoa kiujumla,” alibainisha Kilonzo.
Kilonzo alitaja baadhi ya majina ya wachezaji watakaoshiriki Ligi ya Mkoa kuwa ni Ashura Shaban, Kurwa Daniel, Shakra Ashour, Mwamvita Tabago, Sania Hassan, Pendo Patrick, Veronica Shija, Rehema Charles, Zaituni Maganga, Mwanvita Tabago, Kitenge Nusura, Maombi Mpinda , Rahabu Mfumya, Aisha Amani na wengine.
Pia kocha huyo alitoa mwito kwa viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo wabunge wa Mkoa wa Kigoma wajitambue kwa kutoa michango kwa timu za wanawake ikiwa na lengo la kuhamasisha michezo kwa siku za usoni.




No comments:
Post a Comment