NA YEREMIAS NGERANGERA…NAMTUMBO
Baraza
la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma
limepitisha kwa kauli moja kuwa jina la Sekondari ya wasichana ya mkoa
wa Ruvuma inayojengwa katika wilaya ya Namtumbo kuitwa SAMIA GIRLS
SECONDARY SCHOOL.
Akiwasilisha salamu za serikali katika baraza
la madiwani pamoja na mambo mengine mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma Dkt Julius Kenneth Ningu alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha
shilingi bilioni 3 za kujenga sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma
katika wilaya ya Namtumbo.
Dkt Ningu aliwaambia waheshimiwa
madiwani kitendo cha ujenzi wa sekondari hiyo inaipa hadhi wilaya ya
Namtumbo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla hali inayotupasa kushukuru kama
ilivyoada kushukuru kwa kufanyiwa jambo jema .
Aidha Dkt Ningu
aliwaomba waheshimiwa madiwani kuridhia jina la sekondari hiyo kuitwa
Samia Girls Secondary School kama shukrani ya wananchi wa Namtumbo kwa
Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
kwa kutoa fedha hizo za kujenga sekondari ya wasichana wilayani
Namtumbo.
Hata hivyo Dkt Ningu aliwaambia waheshimiwa madiwani
kilio kikubwa cha wananchi katika wilaya ya Namtumbo ilikuwa bei kubwa
ya mbolea lakini wanamshukuru mheshimiwa Raisi kwa kukubali kutoa
shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kupunguza bei ya mbolea ili
kuwapunguzia wakulima bei ya mbolea.
Lakini pia Dkt Ningu
aliwaagiza waheshimiwa madiwani kuhakikisha wananchi wanaoishi na silaha
katika maeneo yao kuzisalimisha kwa msamaha mwisho tarehe 30 mwezi huu
septemba 2022 na baada ya hapo wananchi watakao kamatwa na silaha baada
ya tarehe hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao alisema
mkuu wa wilaya huyo.
Diwani wa viti maalumu Zalia Banda
akiongea kwa niaba ya madiwani wenzake walimshukuru Mkuu wa wilaya huyo
kwa namna anavyowapa ushirikiano katika maswala ya maendelea katika
wilaya hiyo na kudai kuwa madiwani wataendelea kushirikiana naye kwa
hali na mali.
Zalia Banda pia aliwasilisha ombi kwa mkuu wa
wilaya kupitisha barua iliyoombwa na waheshimiwa madiwani
inayowasilishwa katika ofisi ya waziri mkuu kuhusu malalamiko ya
wananchi kuhusu kukithiri kwa mifugo katika Halmashauri ya wilaya ya
Namtumbo na kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara na wafugaji huku
waathirika wakubwa ni wakulimwa ambapo Mkuu wa wilaya huyo alikubali
kushughulika ombi hilo.
Naye Diwani wa kata ya mkongo Daniel
Nyambo kwa upande wake alipendekeza mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa
Halmashauri utenganishwe kwa madai kuwa mfumo wa ukusanyaji wa kawaida
wa mapato hautiliwi maanani na badala yake kutegemea mapato yatokanayo
na stakabadhi ghalani.
Nyambo alisema ni vyema mfumo wa
ukusanyaji wa mapato ya kawaida mapato yake yatenganishwe na mapato
yanayotokana na ushuru wa papo kwa papo kutoka uuzaji wa mazao kwa njia
ya stakabadhi ghalani ili waheshimiwa madiwani wajue badala ya
kuunganisha mapato yote.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo Jumma Pandu pamoja na kumshukuru mkuu wa wilaya kwa
ushirikiano kati ya ofisi yake na waheshimiwa madiwani alisema madiwani
wataendelea kuisimamia halmashauri na hawatasita kuchukua hatua kwa
watumishi watakaoenda kinyume katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila
siku.
Shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Ruvuma
iliyopewa jina la Samia Girls Secondary School imejengwa katika kijiji
cha Migelegele mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo ambapo Raisi wa Jamhuri
wa muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitoa kiasi cha shilingi
bilioni 3 ili kujenga majengo hayo.
No comments:
Post a Comment