Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amehutubia Mkutano
wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaondelea Jijini New
York nchini Marekani. Makamu wa Rais ametoa hotuba hiyo akimwakilisha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Akitoa
hotuba hiyo, Makamu wa Rais amesema Tanzania na nchi za Afrika kwa
ujumla zinahitaji mabadiliko ya haki na ya utaratibu katika kufikia
matumizi ya nishati mbadala kwa kuzingatia hali za Maisha ya watu wa
bara hilo wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa
nishati hizo. Ametoa wito wa kuondolewa kwa upinzani dhidi ya ufadhili
wa kimataifa katika utekelezaji wa miradi ya mageuzi katika nchi za
Afrika ambayo inalenga kutumia rasilimali ikiwemo gesi kwaajili ya
nishati na matumizi mengine katika kufikia maendeleo.
Makamu wa
Rais ameongeza kwamba biashara ya hewa ukaa barani Afrika inapaswa
kufanyika kwa uwazi na kuwanufaisha wananchi waliotunza mazingira na
misitu inayozalisha hewa hiyo kwa matumizi ya dunia huku akiitaja
Tanzania kama nchi iliowekeza zaidi katika uhifadhi wa misitu ambapo
asilimia 30 ya eneo la ardhi ya taifa hilo imehifadhiwa.
Katika
kudumisha amani na usalama, Makamu wa Rais amesema Tanzania siku zote
inaamini kuwa diplomasia na meza za mazungumzo ndiyo chombo bora cha
kutatua migogoro duniani. Amesema licha ya migorogoro iliopo duniani
mataifa yanapaswa kulinda maisha ya binadamu hasa watoto na wanawake
pamoja na ustawi wa watu. Aidha ameongeza kwamba ni muhimu kushiriki
katika kutafuta utatuzi wa migogoro kwa amani ili kukabiliana na athari
zitokanazo na migogoro hiyo kama vile ongezeko kubwa la bei za chakula
na mafuta pamoja na kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na viwanda duniani
kote.
Makamu wa Rais amesema katika kulinda amani Tanzania
inajivunia kuchangia Askari katika misheni 5 kati ya 16 zilizopo za
kulinda amani duniani kote na kueleza kwamba taifa lipo tayari kuchangia
zaidi iwapo itaombwa kufanya hivyo na kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa
kuongeza uungaji mkono wake kwa juhudi za kikanda katika za kujenga na
kulinda amani.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kuchelewa
kwa Afrika katika upatikanaji wa chanjo za Uviko19 wakati wa mlipuko wa
ugonjwa huo kunasisitza hitaji la Nchi za Kiafrika kufanya kazi pamoja
katika ukuzaji wa masuluhisho asilia kupitia utafiti wa pamoja wa
kisayansi. Amesema ugonjwa huo pia uliweka wazi hitaji la kuwekeza zaidi
katika elimu ya afya ya umma hususani dawa za kinga ili kujenga
ustahimilivu wa mtu binafsi ikiwa ni pamoja na usawa wa mwili, lishe
bora na tabia.
Pia Makamu wa Rais ameshuruku misaada wa
kimataifa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kukabiliana na
kuenea kwa janga la Uviko19 kupitia utoaji wa vifaa vya uchunguzi, dawa,
programu za msaada wa chanjo, ambazo zimekuwa muhimu katika kushinda
vita dhidi ya janga hilo.
Vilevile Makamu wa Rais amepongeza
juhudi za Umoja wa Mataifa katika kukuza lugha ikiwemo tamko la
kihistoria la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO)
lililoitaja "7 Julai" kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Ametoa
wito kwa mataifa kuweka vipaumbele vya vitendo hasa kwenye malengo ya
maendeleo endelevu ambapo amayasihi mataifa kujitolea kufanya kazi kwa
karibu na Umoja wa Mataifa na Nchi Wanachama wake, kwa nia ya
ushirikiano na mshikamano wa kimataifa kuelekea mustakabali endelevu.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip
Mpango akihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA)
unaondelea Jijini New York nchini Marekani.
Friday, September 23, 2022
New
MAKAMU WA RAIS DKT MPANGO AMUWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA BARAZA KUU LA 77 LA UMOJA WA MATAIFA (UNGA),NEW YORK NCHINI MAREKANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment