Na Benny Mwaipaja, Dubai
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu
zimetia saini mkataba wa makubaliano ya kuondoa utozaji Kodi Mara
Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo mbili,
yaani Agreement on Avoidance of Double Taxation and Prevention of Fiscal
Evasion on Income Taxes.
Mkataba
huo umetiwa saini katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Umoja wa Falme za
Kiarabu mjini Dubai na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu
Lameck Nchemba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mhe. Mohamed Bin
Hadi Al Hussain, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Umoja wa Falme za
Kiarabu (UAE)
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa
kusainiwa kwa Mkataba huo ni jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizozifanya Mwezi Februari,
2022 katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo aliagiza kuondolewa
kwa changamoto hiyo ili kukuza mahusiano ya kiuchumi, kuimarisha
ushirikiano katika masuala ya kodi na kuchochea mazingira wezeshi ya
uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
“Ni
matumaini yetu kwamba baada ya mkataba huu ku tutaona uwekezaji mkubwa
ukikua kati ya nchi zetu hizi, hasa kutoka Uarabuni ambao wana mitaji
mikubwa lakini utozaji kodi mara mbili ulikuwa unawakwaza, hata
wawekezaji, wafanyabiashara wa Tanzania wataweza kufanya biashara bila
kuwa na mashaka ya kutozwa kodi mara mbili hivyo kuongeza ukuaji wa
uchumi wa nchi hizi mbili” alisema Dkt. Nchemba.
Dkt.
Nchemba alisema kuwa UAE imeingia mikataba kama hiyo na nchi 139
duniani, zikiwemo nchi za Afrika Mashariki, lakini Tanzania ilikosa
baadhi ya fursa za uwekezaji kutoka mataifa hayo ya Umoja wa Nchi za
Falme za Kiarabu na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo
zinazotokana na kuondolewa kwa changamoto hizo za utozaji kodi mara
mbili.
“Hatua
hii itavutia uwekezaji wa mitaji na ujenzi wa viwanda vitakavyosaidia
kuchakata bidhaa zitakazozalisha ajira kwa vijana wa kitanzania na
itachachua uchumi kwa kuongeza wigo wa kodi, kuongeza uzalishaji wa
bidhaa zitakazo uzwa ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza upatikanaji wa
fedha za kigeni” alisema Dkt. Nchemba
Alisema
kuwa Tanzania imekaa kimkakati kutokana na kuwa lango la biashara
kutokana na uwepo wa bahari, idadi kubwa ya watu, kuwa katika eneo la
kimkakati kijiografia pamoja na kuwa na soko la uhakika katika eneo la
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) linalokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 177.
Hivyo,
kusainiwa kwa mkataba huo kutafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa
kiuchumi ambapo makampuni makubwa yanayomilikiwa na Serikali ya Umoja
wa Falme za Kiarabu yatakwenda kuwekeza nchini Tanzania ambapo
uwekezaji huo utaleta faida katika sekta za uzalishaji, ukuaji wa
viwanda pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Pamoja
na kusaini mkataba huo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alipata fursa ya
kufanya mazungumzo na Waziri mwenzie wa Fedha wa upande wa Umoja wa
Falme za Kiarabu ambapo walizungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano,
ikiwemo ukamilishwaji wa Mkataba wa Kuhamasisha na Kulinda Uwekezaji
yaani “Agreement on Promotion and Protection of Investment” ambapo
walizielekeza timu za wataalam wa pande zote mbili kukutana na kuanza
majadiliano ya mkataba huo kwa faida za pande zote.
Naye
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru,
alisema kuwa kusainiwa kwa Mkataba huo wenye vipengele 31 ambavyo nchi
hizo mbili zimekubaliana kuvitekeleza, utawezesha mtu ama taasisi
inayofanya biashara katika nchi hizo kutozwa kodi ya faida ya mapato
upande mmoja badala ya utaratibu wa awali ambapo walikuwa wakitozwa kodi
hiyo kila upande na kuzua malalamiko kutoka kwa wawekezaji.
“Baadhi
ya watu wanaweza kutafsiri kuwa mikataba ya aina hii ni kusamehe kodi,
lahasha, hii ni mikataba inayoweka kanuni ya kuzuia uhamishaji wa kodi
kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine kwa kuzingatia uwekezaji unatoka
katika eneo gani, inahusisha kulinda mitaji ya wawekezaji wa nchi
husika” alisema Bw. Mafuru
Alisema
kuwa kuwepo kwa mkataba huo kutawejengea wawekezaji uhakika na imani ya
kuwekeza mitaji yao nchini, jambo ambalo halikuwepo huko nyuma, na kwa
kuwa mikataba ya namna hiyo inalindwa kimataifa, na kama kutakuwa na
kutokuelewana kwa namna yoyote, mikataba hiyo itakuwa msingi wa
majadiliano.
Maeneo
yanayoguswa na makubaliano hayo ni utozaji wa kodi katika mapato
yanayotokana na biashara, usafiri wa anga na majini, mali
zisizohamishika, riba, gawio, uvunaji wa rasilimali za asili,
wafanyakazi na watafiti, wanafunzi malipo ya pensheni na Hifadhi ya
Jamii pamoja na masuala ya michezo.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Umoja wa Falme za
Kiarabu, Mhe. Mohamed Bin Had Al Hussain, alisema kuwa hatua iliyofikiwa
ya kuondoa utozaji kodi ya mapato mara mbili kati ya Tanzania na UAE
kutavutia wawekezaji wengi zaidi kutoka katika nchi za Umoja wa Falme za
Kiarabu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa pande hizo mbili.
Alipongeza
jitihada zinazofanywa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha mazingira ya uwekezaji
nchini na kufanikisha jambo hilo la kuondoa utozaji wa kodi ya mapato
mara mbili na kwamba hatua hiyo itavutia mitaji na wawekezaji wengi
kutoka nchi za Kiarabu kuja kuwekeza Tanzania na kuomba pia suala la
kulinda mitaji na uwekezaji lifanyiwe kazi.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Waziri wa
Nchi wa Mambo ya Fedha wa Nchi za Falme za Kiarabu, Mhe. Mohamed Bin
Hadi Al Hussaini, Wakisaini Mkataba wa makubaliano ya Kuondoa Utozaji
Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo
mbili, Mjini Dubai, Falme ya nchi za Kiarabu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Waziri
wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Nchi za Falme za Kiarabu, Mhe. Mohamed Bin
Hadi Al Hussaini, Wakionesha Mkataba wa makubaliano ya Kuondoa Utozaji
Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo
mbili, Mjini Dubai, Falme ya nchi za Kiarabu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa pili
kushoto), na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Nchi za Falme za
Kiarabu, Mhe. Mohamed Bin Hadi Al Hussaini (wa pili kulia), Wakiwa
katika picha ya Pamoja na ujumbe wa Tanzania baada ya kusainiwa kwa
Mkataba wa makubaliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili na Kuzuia
Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo mbili, Mjini Dubai, Falme
ya nchi za Kiarabu. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Lawrence Mafuru na kushoto ni Balozi wa Tanzania Katika
Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu Mhe. Mohamed Mtonga.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto)
akizungumza jambo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Nchi za Falme
za Kiarabu, Mhe. Mohamed Bin Hadi Al Hussaini (wa pili kulia), Ofisi
Ndogo za Wizara ya Fedha mjini Dubai-UAE, kabla ya kusainiwa kwa Mkataba
wa makubaliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa
Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo mbili, Mjini Dubai, Falme ya nchi za
Kiarabu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto)
akiagana na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Nchi za Falme za
Kiarabu, Mhe. Mohamed Bin Hadi Al Hussaini (wa pili kulia), Ofisi Ndogo
za Wizara ya Fedha mjini Dubai-UAE, baada ya kusaini Mkataba wa
makubaliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa
Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo mbili, Mjini Dubai, Falme ya nchi za
Kiarabu.
Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru na Konseli
Mkuu wa Konseli ya Tanzania-Dubai (Balozi Mdogo), Bw. Idi Bakari,
wakifuatilia mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akiagana na Waziri wa Nchi wa
Mambo ya Fedha wa Nchi za Falme za Kiarabu, Mhe. Mohamed Bin Hadi Al
Hussaini (wa pili kulia), Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha mjini
Dubai-UAE, baada ya kusaini Mkataba wa makubaliano ya Kuondoa Utozaji
Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo
mbili, Mjini Dubai, Falme ya nchi za Kiarabu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto)
akipokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Balozi wa Tanzania katika Nchi
za falme za Kiarabu, Mhe. Mohamed Mtonga, katika Jengo la Ubalozi Mdogo
wa Tanzania mjini Dubai. Dkt. Nchemba yuko katika ziara ya kikazi
Uarabuni ambapo Pamoja na mambo mengine amesaini Mkataba wa Makubaliano
ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato
kati ya nchi hizo mbili, Mjini Dubai, Falme ya nchi za Kiarabu.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM-Dubai)
No comments:
Post a Comment