Na Dotto Mwaibale, Singida
WATOTO wa Kanisa la Moravian Tanzania Usharika wa Sabasaba Mkoa wa Singida, wameliombea taifa na viongozi wake wote huku wakiwahimiza wazazi kuendelea kuwapa malezi na matunzo bora.
Wameyasema hayo kwenye Sikukuu yao iliyofanyika katika Kanisa la Moravian Usharika wa Sabasaba mjini hapa sherehe ambayo inafanyika katika makanisa yote ya Moravian hapa nchini kwa utaratibu uliowekwa na kanisa hilo.
Katika ibada ya sherehe yao hiyo watoto hao walimuombea Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wabunge,Spika wa Bunge, Wakuu wa Mikoa na wilaya , Makatibu wakuu na viongozi mbalimbali ili Mungu aendelee kuwapa afya njema na kutumikia Serikali.
Watoto hao mbali ya kufanya maombi hayo walitumia nafasi hiyo kuwaomba walezi na wazazi wao kuendelea kuwatunza na kuwapa malezi bora kwa kuwapa chakula, malazi, mavazi,kuwapeleka shuleni na kanisani ili wakue kiroho, maarifa na kiimani.
"Tunawaomba wazazi wetu wawe wanawaruhusu kuja kanisa ambako tunakutana watoto wote kujifunza mambo mbalimbali na neno la Mungu ili tukue katika imani na kiroho na kuwa watoto bora" alisema Samuel Mwanitu.
Mwanitu alisema kutoa baraka kwa watoto ni jambo jema kwani ndio watakuwa viongozi wajao na akaongeza kuwa Yesu alisema waacheni watoto wadogo waende kwake naye aliwakumbatia na kuwabariki.
Watoto hao katika ibada hiyo walioiongoza waliweza kufanya burudani kwa kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, kusoma vifungu kadhaa vya baadhi ya maneno kutoka kwenye biblia na kutoa zawadi kwa watoto wenzao waliofanya mitihani ya kanisa, zawadi ambazo zilitolewa na mchungaji wa kanisa hilo Oscar Falanga huku muumini wa kanisa hilo Agnes Mwaihojo akiwazawadia walimu wa watoto hao zawadi kutokana na kujitoa kwao kuwafundisha.
No comments:
Post a Comment