Na Happiness Shayo - WMU
Wawekezaji
wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni wanatarajiwa
kukutana jijini Arusha katika Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani
(UNWTO) Kamisheni ya Afrika unaotarajiwa kufanyika Oktoba 5-7, 2022
jijini Arusha.
Maandalizi ya mkutano huo wenye kauli mbiu
inayosema “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo
Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii” yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza
leo katika kikao cha tatu cha kamati ya kitaifa ya maandalizi ya
mkutano huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja
amesema maandalizi yanaendelea vizuri huku akiwaelekeza wajumbe wa
kamati hiyo kuendelea kufanya kazi vizuri ili kufanikisha mkutano huo
kwa viwango vya juu.
“Ninaamini timu hii ni timu iliyokamilika
hivyo kila mjumbe atumie uwezo wake kufanya kazi vizuri ili
tusimuangushe Mheshimiwa Rais,” Mhe.Masanja amesisitiza.
Naye,
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Ndg. Juma Mkomi amesema
Wizara itatoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha mkutano huo na
pia kutatua changamoto zitakazojitokeza.
Mbali na wawekezaji,
mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa UNWTO Ndg. Zurab
Pololikashvili, Waziri wa Utalii wa Ivory Coast Ndg. Siandou Fofana na
mawaziri wa utalii kutoka nchi wanachama wa UNWTO.
Kwa mujibu wa
aya ya 67 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025,
Serikali iliyopo madarakani inaendelea kuweka mkazo katika kupanua wigo
wa bidhaa za utalii ili sekta hiyo iendelee kuchangia katika pato la
Taifa.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Kamati
ya kitaifa ya maandalizi ya Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani
(UNWTO) Kamisheni ya Afrika katika kikao cha tatu kilichofanyika leo
jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Kamati ya kitaifa ya maandalizi ya Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheni ya Afrika katika kikao cha tatu kilichofanyika leo jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment