Na Benny Mwaipaja, Abu Dhabi
Mfuko
wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu umeahidi kutoa
mkopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo
nchini Tanzania ukiwemo mradi wa umeme wa Benaco-Kyaka, mkoani Kagera na
ujenzi wa makazi ya watumishi ya gharama nafuu Visiwani Zanzibar,
inayokadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 420.
Ahadi hiyo
imetolewa Mjini Abu Dhabi na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa
Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al
Suwaidi, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Makao Makuu ya Mfuko huo,
mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mhe. Mohammed Saif
Al Suwaidi alimweleza Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa miradi
mingine ya kimkakati iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania kwenye
Mfuko huo ukiwemo wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius
Nyerere na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itatafutiwa ufadili kupitia
Serikali pamoja na Sekta Binafsi ya nchi hizo kwa kuwa inahitaji
uwekezaji mkubwa wa fedha.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo wa Abu
Dhabi Fund, Mhe. Suwaidi, alisema kuwa Mfuko wake uko tayari kusaidia
pia utekelezaji wa miradi mingine ya kilimo na uvuvi na kwamba fedha
hizo zitapatikana kupitia Kampuni inayojishughulisha na masuala hayo
katika Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Akizungumza na
mwenyeji wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck
Nchemba alikumbushia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi sita
iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania katika Mfuko huo ikiwemo mradi
wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora-Kigoma-Msongati, Ujenzi
wa Bwawa na Julius Nyerere, Mradi wa Umeme wa Benaco hadi Kyaka (220KV)
mkoani Kagera, ujenzi wa nyumba 10,000 za makazi nafuu-Zanzibar, na
mradi wa kuwezesha biashara ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa
kutoka nje.
Aidha, Dkt. Nchemba, aliushukuru Mfuko huo kwa kutoa
fedha kiasi cha shilingi mil. 201 na dola za Marekani milioni 1.3 kwa
ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi
yenye urefu wa kilometa 51.1 kwa kiwango cha lami, barabara ambayo
ujenzi wake umerejea baada ya kukwama kwa muda mrefu.
“Maelekezo
ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
kwamba barabara hii ikamilike mapema ili kuleta manufaa ya kiuchumi na
kijamii kwa pande zote mbili wakiwemo wananchi watakaoitumia barabara
hiyo, na wabunge wa mkoa wa Kigoma wanaisubiri kwa hamu barabara hiyo”
Alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alimweleza Kiongozi huyo kuwa
Tanzania imefungua milango kwa wawekezaji mbalimbali wakiwemo wanaotoka
Abu Dhabi, kwenda kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo
ujenzi wa miradi ya kimkakati, kilimo, mifugo, uvuvi na ujenzi wa nyumba
katika sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo.
“Tumefurahi kwa
kutuahidi kuwa miradi yetu mikubwa ya kimkakati ya kuzalisha umeme, reli
ya kisasa, mmeichukua na kuipeleka Serikalini na kwenye sekta binafsi,
tuo tayari kushirikiana nao na kwa upande wa kilimo na mifugo,
nawahakikishia kuwa ardhi ipo ya kutosha” alieleza Dkt. Nchemba
Kwa
upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
Lawrence Mafuru, alisema kuwa ahadi hiyo ni matunda ya kusainiwa kwa
Mkataba wa kutotoza kodi mara mbili kwenye mapato ya faida pamoja na
udhibiti wa ukwepaji kodi uliosainiwa juzi kati ya Tanzania na Umoja wa
Falme za Kiarabu, mjini Dubai.
Alisema kuwa hatua hiyo itawezesha
wawekezaji wengi zaidi wakiwemo wanaotoka katika sekta binafsi kwenda
kuwekeza nchini Tanzania na kuleta faida za kiuchumi kwa nchi na
wananchi kwa ujumla.
“wao kama Abu Dhabi Fund wanafadhili Sekta
Binasfi ya hapa wanaowekeza katika nchi mbalimbali zikiwemo nchi za
Afrika, kwa hatua tuliyoifanya ya kusaini makubaliano hayo ya kuondoa
changamoto ya utozaji kodi mara mbili, tumefungua fursa nyingine kwa
wawekezaji watakaokuwa wanawezeshwa na Mfuko huu kwenda kuwekeza
nyumbani” Alisema Bw. Mafuru
Alisema kuwa Serikali inatekeleza
mpango wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika utekelezaji
wa miradi ya kimkakati na hivyo ni fursa ya kuvutia mitaji na uwekezaji
kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawekezaji kutoka Abu Dhabi ambao
wameonesha nia ya kuwekeza kwenye kilimo, uvuvi, mifugo na maeneo
mengine.
Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi umetoa fedha kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini Tanzania ukiwemo ujenzi wa
Hospitali ya Wete-Pemba, barabara ya Kidawe hadi Uvinza (km 77), ujenzi
wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera na mradi wa maji Zanzibar vijijini
ambayo imekamilika na hivi sasa wanafadhili ujenzi wa barabara ya
Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi wenye thamani ya dola za Marekani milioni
15.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na
Mwenyeji wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu
Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati
walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania
na Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza
na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund
for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati walipokutana na
kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo,
mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa
katika picha na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu
Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati
walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania
na Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiongozwa
na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund
for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, kuelekea kwenye eneo la
mkutano baada ya kuwasili Ofisi za Makao Makuu ya Mfuo huo, mjini Abu
Dhabi, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu kwa ajili ya mazungumzo kuhusu
ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Mfuko huo.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati),
akiwa katika picha ya Pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa
Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al
Suwaidi (wa tatu kulia), wakati walipokutana na kufanya mazungumzo
kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja
wa Falme za Kiarabu. Wengine ni Balozi wa Tanzania, Umoja wa Nchi za
Falme za Kiarabu Mhe. Mohamed Mtonga (wa pili kushoto), Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (Sera), Bw. Lawrence Mafuru (wa pili
kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha na Mipango Bw.
William Mhoja (kushoto) na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Abu Dhabi Fund
Bw. Adel Abdulla Al Hosan (kulia).(Picha na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini-WFM-Abu Dhabi)
Thursday, September 29, 2022
New
MFUKO WA MAENDELEO WA ABU DHABI KUENDELEA KUFADHILI MIRADI YA MAENDELEO TANZANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment