WENTWORTH GAS LTD ILIVYODHAMIRIA KUKABILI MABADILIKO YA TABIANCHI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, September 25, 2022

WENTWORTH GAS LTD ILIVYODHAMIRIA KUKABILI MABADILIKO YA TABIANCHI

 


-Waweka hadharani takwimu zinaonesha wanavyopunguza hewa ya kaboni

-Sasa kuanzisha mradi wa majiko yanayotumia kuni, mkaa kidogo  

Na Said Mwishehe,

NCHI yetu ya Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani imeendelea kushuhudia athari zinatokana na mabadliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuleta madhara mbalimbali katika maisha ya binadamu.

Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakisababishwa na sababu mbalimbali lakini kubwa ni uwepo wa shughuli za kibinadamu ambazo zimekuwa zikisababisha uchafuzi wa mazingira.

Pia uwepo wa viwanda vikubwa vinavyotumia nishati ya mafuta mazito, gesi na makaa ya mawe navyo vimekuwa vikichangia mabadiliko ya tabianchi.

Uwepo wa mabadiliko ya tabianchi umeifanya dunia kushuhudia kuongeza kwa joto duniani , kumekuwepo na mvua zisizo tabirika na wakati mwingine kusababisha mafuriko makubwa yanayosababisha maafa na uharibifu mkubwa.

Mabadiliko ya tabianchi yemesababisha kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari lakini tunashuhudia baadhi ya misitu mikubwa kwenye mataifa mbalimbali ikiwaka moto.

Ripoti ya Jopo la Wataalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) iliyochapishwa Agosti 9,2021 imesema uchafuzi unaotokana na gesi ya kaboni umepanda kwa kiwango kikubwa duniani.

Kiwango hicho  kinatishia kuvuruga mpango wa kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi wa kuweka viwango vya joto ulimwenguni kusalia nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celsius kufikia mwishoni mwa karne hii.

Na kwamba kiwango hicho kitaongezeka ndani ya kipindi cha miaka 15 ijayo. Ripoti hiyo iliyoidhinishwa na wajumbe kutoka nchi 195 imechapishwa katika wakati ambapo joto kali na mvua kubwa vinashuhudiwa katika mataifa mbalimbali duniani.

Hata hivyo yapo mataifa ambayo yameendelea kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ingawa mataifa mengine yameonekana kusuasua kuchukua hatua stahiki ambazo wameahidi kuzichukua.

 Adha kwa Shirika la Utafiti la Ujerumani la Climate Action Tracker, linaeleza licha ya nchi kadhaa zilizojiunga kwenye mkataba wa Paris wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, kuahidi kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa,bado wanaonekana  kwenda kinyume na ahadi walizotoa.

Jambo kubwa la kufurahisha wakati mataifa mbalimbali duniani yakiendelea kuchukua hatua, tumeona pia wadau wa kampuni na mashirika makubwa yaliyojikita kufanya shughuli za uzalishaji gesi nchini Tanzania yakiweka kipaumbele mikakati ya kupunguza hewa ukaa.

Miongoni mwa wadau hao ni Kampuni ya kimataifa ya Wentworth Gasi Ltd  inayoongoza kwenye uzalishaji wa gesi asili nchini Tanzania na mtambo wao mkubwa wa kuzalisha gesi uko Mnazi Bay katika ufukwe wa Bonde la Ruvuma Kusini mwa Tanzania na shughuli zao zinasaidia kubadilisha uchumi wa siku zijazo.

Pamoja na mambo mengine , Wentworth Gas Ltd inaeleza ripoti yao ya mwaka 2021 waliyoizindua Agosti mwaka huu inaeleza data zao za uzalishaji wa gesi joto kutoka katika mitambo yao ya Mnazi Bay zilikokotolewa kwa kuzingatia kanuni za gesijoto na ni za uhakika mkubwa.

Ofisa  Mtendaji wa Wentworth Katherine Roe anaeleza kwa kina hatua ambazo wanachukua kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa katika tasnia yao na kwamba  wanatarajia kuzindua miradi ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya kaboni mwaka 2022 ili kuendelea kupunguza kiwango cha uchafuzi wa mazingira yao.

“Pia tunatarajia kuimarisha utoaji wa taarifa za shughuli zetu za masuala ya mazingira kwa kufuata miongozo ya Mamlaka ya maadili  ya fedha iliyounda kikosikazi cha usimamizi wa fedha zinazohusiana na hali ya hewa kinachotarajiwa kuwa sharti la lazima ifikapo 2025.”

Kwa upande wake Meneja wa Wentworth Gas Ltd Khalifa Ngaga anasema  katika eneo la kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa salama kwao yanaanzia tangu kwenye shughuli ambazo wanazifanya za uzalishaji wa gesi asili ambapo kuna taratibu wanazozifuata.

“Tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kuanzia kwenye mtambo wetu ili kupunguza hizo hatua za kuchafua mazingira.Moja ya mkakati tunaochukua kwanza ni usalama wa eneo tunalofanyia kazi ,kama utaangalia hizi Kaboni ambazo tunazitolea taaarifa nyingi zinatokana na uchomaji wa gesi na hili linafanyika sababu ya usalama.

“ Sasa tunachoweza kufanya ili kupunguza uchomaji ule wa gesi tunahakikisha gesi ile inayohitajika kwenda kuchoma ndio inachomwa.Tofauti na sehemu nyingine ambazo labda wanachimba mafuta , sehemu yenye mafuta na gesi lazima iwepo lakini sio lazima sehemu yenye gesi basi mafuta yawepo,”amesema Ngaga.

Anaongeza kwenye mafuta wanachoma gesi kwa kuwa hawaihitaji lakini wao gesi ndio mtaji wao kwa hiyo wanaichoma pale inapolazimika hasa ikiwa imezidi kwenye mitambo.

Ameongeza katika mkakati wao wa kupunguza hewa ya Kaboni inayotokana na gesi pamoja na kuwa na jenereta kwa ajili ya shughuli zao za kila siku  kwa sehemu kubwa wanatumia nishati ya umeme wa TANESCO ili kusaidia kupunguza hayo matumizi ya gesi na mafuta ya dizeli kwenye jenereta.

“Pia tunajaribu kutafuta mitambo au vifaa vinavyoweza kupunguza matumizi ya nishati ya gesi na mafuta katika shughuli zetu, kama  tulikuwa tunahitaji q fit Q nane kwa siku labda ukiwa umefunga mtambo mwingine unaoweza kusaidia tunaweza kupunguza gesi inayohitajika kutumika kwenye jenereta.”

Aidha amesema kuna njia nyingi ya kupunguza hiyo hewa ukaa ni kuanzisha miradi ya kijamii inayoweza kusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira.Mradi ambao tunakwenda kuanzisha kwa kushirikiana na washirika wetu ni majiko yanayotumia mkaa au kuni kidogo.

“Majiko ambayo yatatumia kuni chache na chakula kikaiva ndani ya muda mfupi,kwa mfano kama kwa siku ulikuwa unatumia kuni nane kwa ajili ya kupikia , basi sisi tutatoa majiko ambayo utatumia kuni mbili kwa siku na chakula kikaiva.

“Kwa hiyo kama ulikuwa kila baada ya siku mbili uende kukata kuni unaweza kukaa wiki nzima bila kwenda kukata kuni nyingine ,hivyo kwa namna moja au nyingine tutakuwa tumesaidia kupunguza ukataji wa miti.

“Mbali ya majiko yanayotumia kuni chache tutakuwa na mtambo wa kuchemsha maji ya moto na mitambo hiyo itatolewa bure .Kama ulikuwa unakata kuni kwa ajili ya kuchemsha maji kupitia mitambo hiyo hutahitaji tena kukata kuni,”amesema.

Alipoulizwa iwapo kuna uwezekano wa kuachana na matumizi ya gesi, mafuta mazito na makaa ya mawe kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, amesema katika hali ya kawaida gesi huwezi ukaitoa moja kwa moja ,hata hivyo vifaa vingine vinavyotumia mafuta kama kwenye magari na mitambo mingine.

“Katika  hali ya kawaida huwezi kukata kwa mara moja kutumia gesi au mafuta kwa hiyo lazima kuwe na mchakato wa kupitia ili hata unapoondoa ukasema labda ifike mwaka 2050 ndio tunaweza tukafikia.Kwa sasa kuna tatizo linaloendelea kati ya Urusi na Ukraine, Urusi ndio msambazaji mkubwa wa gesi .Nchi ya Ujerumani walikuwa wanasema  wanasema ifikapo mwaka  2030 iwe mwisho kuondoa Makaa ya mawe.

“Sasa hivi  wanafikiria kuanzisha mitambo yao inayotumia Makaa ya mawe kwasababu tayari kuna upungufu.Hata hivyo kama  utaweka Makaa ya mawe , gesi, mafuta mazito na umeme na vitu vingine hewa ya ukaa inayozalishwa na gesi ni ndogo zaidi kuliko inayozalishwa kwenye vitu vingine.”

Hivyo ushauri wake anasema jitihada lazima zifanyike kwa maana ya Serikali, kampuni, mashirika, taasisi na watu binafsi katika uanzishwaji wa hizo nishati jadidifu kama njia sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaweza kutumia umeme unaotokana na maji  au kutumia Sola power  na hizo jitihada lazima ziendelee kufanyika , hata sisi kama Kampuni tunalazimika kutokana na hayo mahitaji ya uzalishaji wa nishati ambayo haichafui mazingira.

“Pia tunalazimika tufikirie kwenye nishati jadidifu tunaweza kufanya nini ,kama  utakumbuka au mmesikia kwenye news Kampuni kubwa kama Shell  wote wameweka ahadi watafanya kile wanachoweza kupunguza hizo athari ,hivyo kupunguza haina maana ndio kuachana  na gesi, mafuta au makaa ya mawe kwa mara moja.

“Bali unaweza kupunguza kwa maana ya wewe kufanya kitu kingine kitakachoondoa kile kiasi ambacho umechafua .Kwetu sisi Wentworth Gas Ltd tumeendelea kupunguza kiwango cha asilimia ya hewa ukaa na ili kupunguza hiyo hewa ukaa lazima kuna vitu vya kuangalia,”amesema Meneja huyo wa Wentworth.

Amefafanua kutokana na hatua mbalimbali ambazo wameendelea kuchukua katika kipindi cha mwaka 2020/2021 wamepunguza kiwango cha hewa ukaa kwa asilimia 10.

“Tunawajibika kama kampuni iliyosajaliwa kwenye soko la hisa na washirika  wetu wanataka kuona tunafanaya jitihada kupunguza hewa ukaa ili kuweza kupunguza hizo athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Ndio maana tunahakikisha mitambo yetu inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ili ifanye kazi kwa ufanisi.

“Mitambo inaposhindwa kufanya kazi kwa ufanisi uwezekano wa kutumia gesi nyingi ni mkubwa , kwa hiyo tunahakikisha mitambo yetu inazalisha kwa ufanisi kwa maana ya kuweza kufanyia mtengenezo ya mara kwa mara kila inapohitajika, na wakati mwingine hatusubiri muda wa kufanya matengenezo.”

Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi amesema hata kwenye kampuni yao imekuwa ikiathirika na mabadiliko hayo kwani nao wanaishi kwenye dunia hii hii.

Amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha nyakati fulani hata wao kuathirika katika shughuli zao.“Kuna wakati eneo ambalo tunafanyia kazi  mvua zilikuwa nyingi hivyo ikasababisha  mmomonyoko wa udongo.

“Kwa hiyo  ilibidi kushirikiana na wadau wetu ambao ni Serikali turekebishe.Kumbuka hatukuwa tumepanga kufanya marekebisho hayo lakini hatukuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuingia gharama kurudisha mazingira sawa sawa.”

Meneja wa  Wentworth Gas Ltd, Khalifa  Ngaga (wa pili kulia) alipokuwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya Mipango Endelevu ya Kampuni hiyo.Wengine ni maofisa wa Kampuni hiyo .(PICHA NA MAKTABA YETU).


Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wentworth Katherine Roe alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Mipango Endelevu ya Kuwezesha Watu kwa Nishati ya mwaka 2021 . Ripoti hiyo ilizinduliwa jijini Dar es Salaam.Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imeelezea hatua zinazochukuliwa na kampuni hiyo kupunguza hewa ya kaboni kama njia ya kukabiliana na athari za mabadiliano ya tabianchi nchi.

No comments:

Post a Comment