KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali kupitia
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuwezesha vijana wa
kitanzania kusimamia na kuendesha mitambo ya kuchakata gesi nchini
ambayo imewezesha gesi hiyo kusafirishwa kwa ajili ya matumizi
mbalimbali ikiwemo kwenye mitambo ya kuzalisha umeme, viwandani,
majumbani na kwenye magari.
Pongezi
hizo zimetolewa tarehe 11 Oktoba 2022, baada ya Wajumbe wa Kamati hiyo
kufanya ziara katika visima vya gesi katika Kijiji cha Mnazi Bay na
Msimbati pamoja na kiwanda cha kuchakata Gesi Asilia katika eneo la
Madimba mkoani Mtwara. Ziara hiyo ililenga kujihakikishia kuwa shughuli
za uzalishaji gesi pamoja na miundombinu yake inafanya kazi
inavyostahiki.
“Kwa
mfano kituo hiki cha Madimba ni muhimu sana kwa sekta yetu ya gesi
nchini na kinaendeshwa na watanzania wenyewe katika mfumo mzima wa
kuchakata gesi, Tunaipongeza Serikali kwa kuhakikisha kuwa maeneo kama
haya yenye uwekezaji mkubwa yanaendeshwa na kumilikiwa na watanzania
wenyewe.” Alisema Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dunstan Kitandula
Alisema
kuwa, gesi iliyopo inatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umeme
ambapo zaidi ya asilimia 60 ya umeme nchini unazalishwa kwa kutumia Gesi
Asilia na kuongeza kuwa, matumizi ya gesi yameongezeka hivyo ameiasa
Serikali kuvutia uwekezaji zaidi na kuchimba gesi zaidi ili kukuza
uchumi wa nchi.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt.James Mataragio, alisema
kuwa, mitambo ya kuchakata gesi ya Madimba inachakata gesi futi za ujazo
milioni 210 kwa siku ambazo husambazwa kwa bomba kwenda maeneo
mbalimbali ikiwemo ya viwanda, majumbani na kwenye mitambo ya umeme.
Alieleza
kuwa, matumizi ya Gesi Asilia yanazidi kuongezeka hivyo Shirika hilo
limejiandaa kuzalisha gesi zaidi ili kuweza kuwa na gesi ya kutosha kwa
ajili ya matumizi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment