Na Innocent Mungy, Bucharest
TANZANIA
imechaguliwa miongoni mwa nchi 48 kati ya nchi 193 wanachama wa ITU
kuwa katika Baraza la Shirika la Mawasiliano duniani - International
Telecommunication Union (ITU) kwa mwaka 2023 hadi 2026. Tanzania ni
miongoni mwa nchi 13 zinazowakilisha Bara la Afrika.
Baraza
la ITU ni chombo cha Shirika la Mawasiliano Duniani chenye mamlaka ya
kusimamia masuala ya kisera ya mawasiliano ya simu ili kuhakikisha kuwa
shughuli za ITU, sera na mikakati inasimamiwa kikamilifu kwa kuzingatia
mazingira ya mawasiliano leo yanayobadilika kwa kasi.
Mheshimiwa
Nape Nnauye (Mbunge), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari Tanzania amethibitisha dhamira ya Tanzania katika ITU kwa miaka 4
itakayokuwa katika Baraza hilo.
"Napenda
kusisitiza kuwa Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi nyingine
wanachama, Sekretarieti ya ITU na ofisi za Kanda ili kuifanya ITU kuwa
chombo muhimu cha kimataifa ambacho kina mchango mkubwa katika
kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zote wanachama kama
mjumbe wa Baraza la ITU" alisema Mhe.Nnauye.
Baada
ya kumchagua Doreen Bogdan-Martin (Marekani) kuwa Katibu Mkuu wa ITU,
na Tomas Lamanauskas (Lithuania) Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi 3
wanaosimamia maeneo matatu ya msingi ya kazi za ITU, nchi wanachama wa
Shirika hilo la ITU wamekamilisha uchaguzi wa Baraza Kuu la ITU na Bodi
ya Kanuni za Redio.
Mario
Maniewicz (Uruguay) alichaguliwa kuhudumu kwa muhula wa pili kama
Mkurugenzi wa Sekta ya Mawasiliano ya Redio ya ITU, ambayo ina jukumu la
kudumisha na kutekeleza mkataba wa Kanuni za Redio unaowianisha
matumizi ya wigo wa kimataifa na mizunguko ya satelaiti, na kwa
kuendeleza viwango vya kiufundi vinavyohusiana.
Seizo
Onoe (Japan) amechaguliwa kuongoza Sekta ya Viwango vya Mawasiliano ya
ITU, ambayo ina uanachama wa serikali, mashirika, na wataalam wa
kiufundi kutoka duniani kote na inasimamia kuunda na kusimamia viwango
vya kiufundi vya kimataifa vya mawasiliano ya simu na TEHAMA.
Dkt.
Cosmas Zavazava (Zimbabwe) amechaguliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Sekta
ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU, ambayo inasimamia kuratibu juhudi za
kimataifa za kuunganisha wasiounganishwa kupitia kuhamasisha maendeleo
ya kidijitali yenye usawa na jumuishi, kuimarisha uwezo na miundombinu
ya mataifa yanayoendelea, na kuzindua mipango ya kufanya teknolojia
iweze kupatikana kwa kila mtu.
Wajumbe
12 walichaguliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Kanuni za Redio ITU. Ofisi
hiyo inasimamia kudumisha na kutekeleza mkataba wa Kanuni za Redio,
ambao unaunganisha matumizi ya wigo wa kimataifa na mizunguko ya
satelaiti, pamoja na kuunda viwango muhimu vya kiufundi.
Kuanzia
Januari 1, 2023, viongozi watano waliochaguliwa pamoja na Wajumbe 48 wa
Baraza la ITU wataanza uongozi wa miaka minne hadi 2026.

No comments:
Post a Comment