Na Benny Mwaipaja, WFM
Ujerumani
imepatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni 210 kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya sekta za afya, maji, utalii, mazingira, utawala
bora, kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuboresha mfumo wa
kidijitali kwa ajili ya kufuatilia matukio ya vitendo vya ukatili kwa
wanawake na watoto.
Ujerumani imetangaza uamuzi huo mjini Berlin
baada ya kukamilika kwa majadiliano kati ya ujumbe wa Tanzania
ulioongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck
Nchemba na Ujumbe wa Ujerumani ulioongozwa na Naibu Waziri anayesimamia
uhusiano wa kiuchumi na Maendeleo wa nchi hiyo, Dkt. Barbel Kofler.
“Serikali
ya Tanzania inafuraha kupokea msaada wa Euro milioni 87 sawa na
shilingi za Tanzania bilioni 210, utakaosaidia kwa kiwango kikubwa
kuboresha Maisha ya watu” alisema Dkt. Nchemba wakati akitoa neno la
shukrani baada ya kusainiwa kwa nyaraka za makubaliano ya msaada huo.
Dkt.
Nchemba alifafanua kuwa msaada huo utaelekezwa kutunza baioanuai ya
Hifadhi za Taifa na maeneo ya uwindaji ili kutunza mazingira ya maeneo
hayo kwa kuongeza mapato na kuwa na utalii endelevu.
“Msaada huo
pia unakusudia kuboresha afya ya mama na mtoto, kuimarisha uzazi wa
mpango hususan kwa vijana na mpango wa bima ya afya kwa wote” alieleza
Dkt. Nchemba
Alisema kuwa eneo lingine ambalo fedha hizo
zitaelekezwa ni pamoja na usafi wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya
maji ili kuwawezesha watu wengi kupata maji safi na salama ya kunywa
Tanzania Bara na Visiwani.
Dkt. Nchemba alisema kuwa sehemu ya
msaada huo pia itaelekezwa kwenye jamii ikiwemo usawa wa kijinsia,
kuimarisha haki za wanawake na Watoto kwa kuzuia kila aina ya vitendo
vya ukatili dhidi yao ili kuharakisha maendeleo ya nchi
Alisema
kuwa usimamizi na utawala bora wa fedha za umma, na kuboresha mifumo ya
fedha ni miongoni mwa faida zitakazotokana na msaada huo pamoja na
sehemu ya fedha hizo kutumika katika masuala ya utafiti na uandishi wa
miradi inayokusudiwa kutekelezwa na serikali kupitia mfuko wa mafunzo na
utaalam.
Dkt. Nchemba alifafanua Zaidi kuhusu miradi
itakayonufaika na fedha hizo kuwa ni mradi wa Hifadhi ya mfumo wa
ikolojia wa Serengeti, Mradi wa Hifadhi ya ikolojia ya Selous na
Nyerere, mradi wa kuboresha afya Tanzania awamu ya pili, kuimarisha haki
za wanawake na Watoto, kujenga kituo cha mfumo wa kidijitali kwa ajili
ya taarifa za haki za raia na usawa wa kijinsia, mradi wa usalama wa
maji maeneo ya mijini Tanzania Bara na Zanzibar, kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi pamoja na masuala ya utafiti na utaalam.
“Kwa
niaba ya Serikali ya Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan, ninaishukuru Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kwa
msaada huu mkubwa na nikuhakikishie kuwa tutafuatilia matumizi ya fedha
hizi kwa karibu zaidi ili manufaa yaliyokusudiwa yapatikane” alisisitiza
Dkt. Nchemba.Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu lameck Nchemba (Mb) akisaini
nyaraka za makubaliano ya msaada wa shilingi bilioni 210 ambazo
Ujerumani imeipatia Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya sekta
za afya, maji, utalii, mazingira, utawala bora, kuwawezesha wanawake
kiuchumi pamoja na kuboresha mfumo wa kidijitali kwa ajili ya kufuatilia
matukio ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto. Kulia ni Naibu
Waziri anayesimamia uhusiano wa kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Dkt.
Barbel Kofler.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu lameck Nchemba (Mb) akizungumza
jambo wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya msaada wa shilingi
bilioni 210 ambazo Ujerumani imeipatia Tanzania kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi ya sekta za afya, maji, utalii, mazingira, utawala bora,
kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuboresha mfumo wa kidijitali
kwa ajili ya kufuatilia matukio ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na
watoto. kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi.
Amina Shaaban na kulia ni Naibu Waziri anayesimamia uhusiano wa kiuchumi
na Maendeleo wa Ujerumani, Dkt. Barbel Kofler.
Friday, November 18, 2022
New
UJERUMANI YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SH. BILIONI 210
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment