NA MWANDISHI WETU
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA) kwa mara nyingine tena limeshinda tuzo ya Ubora ya
Kimataifa ya mwaka 2022 – (Eurpopean Award for Quality Choice
achievement 2022) katika daraja la Diamond inayotolewa na Jumuiya ya
Ulaya inayojishughulisha na utafiti wa ubora – European Society for
Quality Research (ESQR).
Tuzo hii ambayo imepokelewa usiku wa
jana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Massana Mwishawa -
Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Beatrice
Kessy anayesimamia Maendeleo ya Biashara wakiwa na wenyeji wao Kaimu
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Juma Salum, Vivian Rutaihwa, Stella
Mkude katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na ESQR katika
Hotel ya Le Plaza jijni Brussels, Ubelgiji.
Hii ni ni tuzo ya
tatu kutolewa na taasisi hii kwa TANAPA ambapo tuzo ya kwanza ilitolewa
mwaka 2022 – “Best Practice Award – GOLD category, mwaka 2021 ilipata
tuzo ya “Quality Achievement – PLATINUM category na mwaka huu 2022
inapokea tuzo ya Quality Choice – DIAMOND category.
Kwa mujibu
wa Mkurugenzi Mtendaji wa ESQR, Michael Harris jumla ya kampuni na
taasisi 41 kutoka nchi 31 duniani zimeshirikishwa katika kinyang’anyiro
hiki ambapo kwa Tanzania ni TANAPA pekee imeshirikishwa.
“TANAPA
imekuwa mshindi wa tuzo ya ubora wa juu katika uhifadhi na huduma za
kiutalii” Bwana Harris alitangaza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo.
Naye
kaimu Balozi wa Tanzania katika Jumuiya ya Ulaya, Ubeligiji na
Luxembourg, Bwana Juma Salum aliipongeza sana TANAPA kwa kazi
iliyotukuka ya uhifadhi na huduma za utalii kufikia kiwango cha
kutambuliwa na jumuiya za kimataifa.
Kamishina wa Uhifadhi wa
TANAPA, Bwana William Mwakilema alisema inatia moyo kuona jitihada za
wahifadhi walioko katika hifadhi za taifa zimetambuliwa na jumuiya ya
kimataifa.
“Bila shaka tuzo hii itachochea mioyo ya wahifadhi wetu kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu zaidi” Bw. Mwakilema alisema.
Kamishina
Mwakilema alisema pia tuzo ya ubora wa juu itawapa imani watalii na
wawekezaji juu ya utendaji bora wa nchi yetu katika myanja ya uhifadhi
na utalii.
“Nina imani hii tuzo itakuwa na mchango katika
jitihada za Rais wetu Mama Dkt Samia Suluhu Hassan za kuvutia watalii
milioni tano kufikia mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya
Chama cha Mapinduzi” Mwakilema alisisitiza.
No comments:
Post a Comment