NA WAF, DODOMA
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe
amewataka wataalam wa TEHAMA kufanyia kazi mifumo ya taarifa ya Wizara ili
iweze kuwasiliana na kuwa na mifumo michache yenye kuleta tija na kurahisisha
utoaji wa huduma.
Dkt. Shekalaghe amesema hayo alipokuwa akifungua
kituo cha umahiri katika masuala ya afya kidigitali Jijini Dodoma.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza
kuanza kwa matumizi ya tiba mtandao lakini pia ameelekeza kwamba lazima mifumo
yetu ipungue, ninafurahi siku ya leo ni moja ya hatua ya utekelezaji wa
maelekezo ya Mhe. Rais. Wataalam wetu wakikaa hapa wataweza kuja na suluhisho
la changamoto za mifumo iliyopo na kuwa na mifumo michache yenye tija” amesema
Dkt. Shekalaghe
Amesema, kituo hicho cha umahiri katika masuala ya kidigitali (CDH) kitasaidia kuunganisha mifumo ya Sekta ya Afya pamoja na kupunguza mifumo iliyopo katika Wizara ya Afya.
“Kituo hiki kitasaidia kupungua kwa mifumo mingi ambayo haitazidi mifumo Minne au Mitano lakini pia kuwezesha kuunganisha mifumo iliyopo kwa kuweza kusomana ndani ya Wizara ya Afya”, amesema Dkt. Shekalaghe
Vile vile, Dkt. Shekalaghe amesema kuwa taarifa zinazotolewa na kituo hicho ziweze kutumika kwa ajili ya tafiti zitakazotuwezesha kufanya maamuzi mazuri zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la PATH Bw. Amos Mugisha amesema wamewezesha kukarabati wa kituo hicho, kuweka samani pamoja na vifaa vya kiteknolojia.
Amesema, moja ya umuhimu wa kituo hicho ni kuweza kutengeneza mifumo ambayo inazungumza na kupunguza mifumo mingi iliyopo katika Sekta ya Afya kwa sasa.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA Wizara ya Afya
Bw. Silvanus Ilomo amesema kuwa kituo hicho kitatumiwa siyo tu na Wizara ya
Afya bali wataalam wengine wa Sekta ya Afya kwa ajili ya kukutana na kuja na
mifumo yenye tija katika uboreshaji wa huduma za afya nchini.
“Kituo hiki ni mali ya Serikali, wataalam wote wa
Sekta mnakaribishwa kuja kufanya kazi hapa kwa kuwa hii ni Serikali moja na
haya ni mafanikio ya Serikali hii”, amesema Bw. Ilimo.








No comments:
Post a Comment