NA SELEMANI MSUYA
NCHI za Afrika zimeshauriwa
kuwekeza katika utafiti wa mbegu asili kwa kuwa zina lishe bora, uhakika wa
chakula na salama kwa afya ya mtumiaji.
Ushauri huo umetolewa na wadau
mbegu asili kutoka nchi 25 za Bara la Afrika, Marekani na Ulaya ambao
wanakutana jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kujadili hatma ya mbegu asili
katika nchi zao na dunia kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano huo
Paul Chilewa kutoka Mwamvuli wa Asasi za Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM),
alisema mkutano huo ambao umehusisha zaidi ya watu 100 kutoka nchi 25 ni muhimu
kwa wadau wote wa mbegu asili kujadiliana namna ya kuzilinda mbegu za asili.
Chilewa amesema Afrika kwa sasa
ina changamoto kubwa ya mbegu za asili, hali ambayo itachangia kukosekana kwa
uhakika wa chakula kwa siku nyingi.
“Mbegu asili zina lishe nyingi
na salama kwa afya ya mtumiaji, hivyo ili kuhakikisha zinakuwa endelevu ni
lazima kufanyika tafiti ambazo zitaonesha ni namna gani tunaweza kuzilinda,”
alisema.
Ofisa huyo alisema iwapo
Serikali itafanya utafiti ambao utashirikisha wakulima ambao wanatumia mbegu
asili ni wazi kuwa changamoto hiyo itapata jibu sahihi.
Chilewa alisema iwapo
hakutakuwa na juhudi za kukabiliana na changamoto ya mbegu asili, ni wazi kuwa
wakulima wataingia kwenye mtego wa kununua mbegu ambazo zitahitaji viuatilifu
na mbolea ambavyo vina sumu na kusababisha maradhi mbalimbali.
Mratibu wa Mratibu wa Mtandao
Baionoai Tanzania (TABIO) Abdallah Mkindi, amesema utafiti unaonesha asilimia
80 ya wakulima wa Afrika wanatumia mbegu asili, hivyo ni muhimu kuhamasisha
matumizi ya mbegu hizo.
Amesema pia utafiti umeonesha
mbegu asili zina virutubisho, hivyo iwapo jamii itahamasishwa kutumia mbegu hizo
changamoto ya utapiamlo ambayo inakabili mataifa hayo itapata muafaka.
“Mbegu asili zina nafasi kubwa
ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameonesha madhara makubwa
duniani, hivyo rai yangu ni kuziomba serikali za Afrika kutenga fedha zitakazotumika
kufanya utafiti wa mbegu hizi,” alisema.
Mkindi alisema TABIO kwa
kushirikiana Mtandao wa Uhuru wa Chakula Dunia (AFSA) na SwissAid
wamewakutanisha wadau hao ili waweze kujadiliana na kutoka na kauli moja kuhusu
hatma ya mbegu asili ambazo zinaonekana kupewa kisogo na watunga sera na
sheria.
Kwa upande wake Mbunge wa Lindi
mjini, Hamisa Abdallah alisema kilimo cha mbegu asili ndio kinaweza kuleta tija
kwenye sekta hiyo, kwani historia inaonesha wazee wa zamani walitumia njia
hiyo.
Hamida alisema mbegu asili
hazina gharama kwenye kilimo kama ilivyo kilimo cha kisasa, hivyo ni wakati
muafaka wa jamii kurejea katika mfumo huo wa zamani.
Alisema kutokana na madhara
ambayo yanapatikana kwenye kilimo cha kisasa, dunia imeanza kubadilika na
kutaka kurejea mifumo ya zamani ambayo ilijikita katika mbegu za asili.
“Mimi naishi na wakulima wa
hali ya chini ambao anashirikiana nao kuendeleza matumizi ya mbegu asili, hivyo
anaungana na wadau wengine ambao wanataka uwekezaji katika utafiti wa mbegu
hizo ambazo ni salama kwa afya ya binadamu,” alisema.
Alisema mkutano huo ni ujumbe
sahihi kwa viongozi duniani kuweka mkazo wa kusisitiza kilimo kinachojikita
katika mbegu asili ambazo ni salama kwa afya ya binadamu na mazingira.
Hamida alisema tafiti
zinaonesha kuwa hata ongezeko la magonjwa dunia kwa sasa sababu kubwa ni jamii
kuacha kutumia mbegu asili kwenye kilimo.
“Sisi Lindi tumefungua benki ya
mbegu asili, hiyo ikiwa ni kuonesha ni namna gani tumejipanga kuachana na mbegu
za kisasa ambazo zina madhara mengi kwenye afya ya binadamu,” alisema.
Mbunge huyo alisema atumia
nafasi yake ya ubunge kuzungumzia na kushawishi umuhimu wa mbegu asili kwenye
kilimo.
Mwakilishi wa Wizara ya Kilimo,
Beatrice Banzi alisema Tanzania imekuwa ikihamasisha watafiti kufanya utafiti katika
sekta hiyo ya mbegu asili na mbegu zingine.
Alisema kilio cha dunia ni
uwepo wa mbegu bora na salama kwa afya ya binadamu, hivyo utafiti pekee ndio
unaweza kutoa jibu.
Ofisa Program wa AFSA, Famara
Diédhiou alisema ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika kuungana kuhakikisha
mbegu asili zinapewa kipaumbele katika sekta ya kilimo.
“Tumekutana hapa Tanzania
nadhani ni wakati muafaka kwa sisi kupigania uwepo wa chakula bora chenye
lishe, kwa kuhamasisha matumizi ya mbegu asili,” alisema.
Katika mkutano huo nchi
zilizoshiriki ni Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Senegali, Burkina Faso,
Ivory Cost, Hispania, Norway, Zambia, Zimbabwe, Australia, Togo, Mali, Benin,
Chad, Tunisia, Niger, Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Misri, Rwanda, DR Congo
na Gabon.








No comments:
Post a Comment