WATOTO 20,000 WENYE USONJI WANAKADIRIWA KUZALIWA NCHINI KWA MWAKA - MAGENDELA BLOG

Recent-Post

ads header

Wednesday, April 2, 2025

WATOTO 20,000 WENYE USONJI WANAKADIRIWA KUZALIWA NCHINI KWA MWAKA


NA MWANDISHI WETU


TANZANIA inakadiriwa kuwa na watoto takribani 20,000 ambao wanazaliwa wakiwa na tatizo la usonji kila mwaka ingawa hakuna takwimu rasmi ya idadi ya walio na changamoto hiyo hiyo sasa.


Hayo yamebainishwa leo, na Naibu Waziri wa Afya, Godwine Molell, wakati akitoa tamko kuhusu Siku ya Usonji Duniani ambayo uadhimishwa Aprili 2, kila mwaka.


Ameongeza kuwa kati ya hao watoto 1416 wanapewa huduma maalum na hiyo inaonesha kuongezeka kwa mahitaji ya msaada wa kipekee kwa kundi hilo.


"Hatuwezi kuzuia wazazi kuzaa watoto wenye changamoto hiyo, kikubwa kinachotakiwa ni kubadilisha mtindo wa maisha ikiwemo kula mlo bora, kufanya mazoezi , kufanya uchunguzi wa Afya mara kwa mara na kuepuka vileo," amesema.



Pia ametoa wito kwa wazazi kuacha kuwaficha watoto wenye usonji na badala yake wawapeleka katika vituo vya huduma ili wapate matibabu na elimu inayostahili.



Amesema kwa sasa Serikali inaendelea na mikakati  ya kuboresha huduma za afya na elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha wanapata fursa sawa kama watoto wengine.


“Tunaendelea kuimarisha huduma kwa watoto wenye usonji kwa kuongeza wataalamu wa afya kama watoa tiba kwa vitendo, physiotherapists na wataalamu wa lugha na matamshi. 


Pia, serikali inawekeza kwenye shule maalum kwa ajili ya watoto hawa,” alisema Dkt. Molell.


Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha mafunzo ngazi ya Diploma yanayohusu mbinu na mikakati ya kufundisha watoto wenye usonji na kutambua dalili katika Chuo Cha Ualimu Patandi Arusha.

Amefafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza wahitimu wenye ujuzi stahiki na weledi wa kuwafundisha watoto wenye usonji nchini


Pia  Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza, Dkt. Omari Ubuguyu, amesema miongoni mwa sababu zinazofanya watoto kuzaliwa na tatizo hilo ni wazazi kuwa na umri mkubwa na sababu nyingine ni ile inayotokana na vinasaba.


 Akifafanua zaidi kuhusu Usonji amesema  kuwa ni hali inayoathiri mfumo wa fahamu na ukuaji wa mtoto ambao unasababisha changamoto katika mawasiliano na mahusiano ya kijamii, na mara nyingi hujitokeza kabla ya mtoto kufikisha umri wa miaka mitatu.




“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mtoto mmoja kati ya 100 anaathirika na usonji, huku tafiti zikionesha kuwa watoto wa kiume wanaathirika mara nne zaidi ya watoto wa kike.   



Katika maadhimisho haya, serikali imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma kwa watoto wenye usonji, ili kuhakikisha wanapata elimu na matibabu sahihi kwa maendeleo yao na ustawi wa jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment