TFRA, NLUPC WATEKELEZA MCHAKATO WA URASIMISHAJI MASHAMBA MKOANI SONGWE - MAGENDELA BLOG

Recent-Post

ads header

Tuesday, April 1, 2025

TFRA, NLUPC WATEKELEZA MCHAKATO WA URASIMISHAJI MASHAMBA MKOANI SONGWE


Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent (kulia) akiita majina ya wanakijiji kwa ajili ya kusogea mezani ili kuhakiki taarifa zao kwenye hati miliki za kimila za mashamba wanayomiliki katika kijiji cha Kanga, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani Songwe Aprili Mosi,  2025 

NA MWANDISHI WETU, SONGWE

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa zoezi la urasimishaji wa mashamba kwa wakulima waliosajiliwa mkoani Songwe aliposhiriki kwenye zoezi la uhakiki wa hati miliki za kimila za mashamba ya wakulima wa Kijiji cha Kanga kilichopo katika Wilaya ya Songwe mkoani Songwe. 


Laurent ameonesha kuridhishwa na zoezi hilo Mosi Aprili Mosi, 2025 alipotembelea kijiji hicho kujionea utekelezaji wa zoezi la uhakiki wa hati miliki za kimila za mashamba ya wakulima 3,098 wa vijiji vya Gua, Kapalala, Kanga na Galula linalotekelezwa kwa awamu ya kwanza katika wilaya ya Songwe kwa ushirikiano baina ya TFRA, NLUPC na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.   


Shughuli hiyo linaenda sambamba na uhuishaji na usajili wa wakulima, uchukuaji wa taarifa kwa ajili ya upatikanaji wa kadi janja na uandikishaji wa wakulima kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya taifa (NIDA)


Mkurugenzi Mtendaji huyo ametoa rai kwa wakulima wote waliosajiliwa kujihusisha na kilimo chenye tija kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kutumia pembejeo ili kuongeza tija ya uzalishaji.


Aidha Laurent amewahakikishia wakulima kuwa ni nia ya serikali kuhakikisha wakulima waliosajiliwa na kukidhi vigezo wanapatiwa hati miliki na kadi janja za utambulisho wa mkulima.


Hatua ambayo itamsaidia mkulima kunufaika na umiliki wa ardhi na fursa mbalimbali zikiwemo za kifedha na mikopo.  


Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NLUPC , Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Matumizi ya Ardhi, Rehema Kishoa, amesema ukamilishaji wa hatua hii utawezesha wakulima kukabidhiwa   hati miliki za kimila zitakazowawezesha kuongeza usalama wa ardhi  na  kuiwezesha TFRA  

 kupata taarifa sahihi za mashamba ya wakulima ili kuboresha utoaji wa huduma za pembejeo za kilimo  ikiwemo mbolea na mbegu kwa bei ya ruzuku .


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kanga, Erick Kihinda, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa kipaumbele wakulima wa Mkoa wa Songwe kupimiwa mashamba yao na kupewa hati miliki zitakazowafaa katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususan katika kuendeleza kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo alizeti, mahindi na ufuta.


Aidha Kihinda amempongeza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwa  usimamizi  thabiti wa sekta ya kilimo ambapo wakulima wanashuhudia mabadiliko makubwa  yanayofanyika  kwa lengo la  kuinua uchumi wa taifa na mwananchi mmoja mmoja.


Naye, Ofisa Tarafa wa Tarafa ya Songwe, Godwin Kaunda, amesema serikali inatekeleza majukumu yake kwa wakati kama inavyoahidi.


“Ni mwaka jana tu tulianza zoezi la upimaji wa mashamba lakini leo tunakwenda kuhakiki hati zetu. Urasimishaji wa ardhi unaleta usalama kwa wakulima na kusaidia kuondoa migogoro ya mipaka iliyokuwepo hapo awali’’. amemaliza kusema Kaunda.


Wakulima wakisikiliza maelekezo ya serikali kabda ya kuanza rasmi kwa zoezi la kuhakiki taarifa zao kabla ya kumilikishwa hati miliki za kimila za mashamba wanayoyamiliki katika kijiji cha Kanga Wilayani Songwe mkoani Songwe.


No comments:

Post a Comment