Na Hamisi Magendela
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika ametoa wito kwa klabu kubwa nchini kusaka vipaji kuanzia ngazi ya mtaa.
Mnyika aliyasema hayo wakati akifunga mashindano ya Kombe la Ntinika yaliyoshirikisha timu 20 kutoka mitaa yote ya Kata ya Mbezi.
Alisema endapo timu mbalimbali zingekuwa zina utaratibu wa kushuka katika ngazi za mtaa na kuachana na mtazamo kuwa na wachezaji wenye majina, soka ya Tanzania ingepiga hatua katika mchezo kutokana na vipaji vingi kuwa kwenye ngazi ya mitaa.
“Katika ngazi ya mitaa kuna vijana wengi ambao wanahitaji kupewa msukumo ili waweze kuwa wachezaji wazuri na kulisaidia taifa siku za baadae, hivyo ni vyema timu kubwa zikaanzia kwenye mitaa,alisema Mnyika.
Pia Mbunge huyo alitoa mwito kwa Halmashauri wa Manispaa Kinondoni kuboresha viwanja vya mpira, kwani vijana wengi wanatumia viwanja visivyo na ubora.
Mbunge huyo hakusita kumpongeza mkurugenzi wa mashindano hayo Nicholaus Ntinika kwa kuanzisha mashindano hayo ya ngazi ya mtaa kwa lengo la kukuza vipaji kwa vijana.
Katika mashindano hayo Black Lion iliifunga Home Boys kwa mabao 2-1 na kukabidhiwa kitita cha sh 100,000, jezi seti moja pamoja na kikombe wakati mshindi wa pili alipewa sh 50,000, jezi seti moja pamoja na mpira na mshindi wa tatu alikabidhiwa mipira miwili na sh 20,000.
Monday, December 19, 2011
New
Mnyika: Soka lianzie mitaani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment