Na Zahoro Mlanzi
WAKATI maelfu ya Watanzania wakiwa gizani juu ya kifo cha ghafla cha Msanii mahiri wa Muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva), Albert Mangwea 'Ngwea' (31) kilichotokea Afrika Kusini, Baba Mdogo wa msanii huyo, Mzee Mangwea amesema taratibu za mazishi pamoja na mapokezi yatafanyika Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Msanii huyo alifariki dunia juzi nchini humo katika Hospitali ya Mtakatifu, Hellen Joseph baada ya kushindwa kuamka tangu alivyolala na kulazimika kukimbizwa hospitalini ambapo umauti ulimkuta .
Hata hivyo, mpaka sasa haijajulikana hasa ni kitu gani kilichosababisha kifo cha msanii huyo ambaye alikuwa ni mmoja wa wasanii wanaounda Kundi la 'East Zoo' .
Wasanii wengine waliounda kundi hilo ni Mez B, Noorah na Dark Master.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam jana, baba mdogo huyo wa marehemu ambaye yupo kikazi Mbinga, Songea amewasiliana na Baba Mkubwa wa Ngwea, David Mangwea na watakutana leo kufanya kikao cha familia ili kutoa taratibu za mazishi.
Taarifa hizo zilieleza kwamba watakutana Mbezi Beach ambako taratibu zote za mazishi ikiwemo kupokea wageni zitafanyika huku baba mdogo huyo akipendekeza maziko yafanyikie mkoani Morogoro sehemu alipozikwa baba yake mzazi.
![]() |
| Marehemu, Albert Mangwea 'Ngwea' enzi za uhai wake. |
Baada ya kikao hicho cha familia, taarifa rasmi kuhusu msiba huo zitatolewa pamoja na mambo mengine.
P-Funk atoa neno
Mtayarishaji Mkongwe wa muziki nchini, P Funk 'Majani' amesema hataki Kituo cha redio cha Cloud's Fm kuendelea kupiga nyimbo za msanii huyo alizorekodi katika studio yake katika kipindi hiki ya maombolezo.
Kwa mujibu wa ujumbe mfupi uliowekwa kwenye Mtandao wa Kijamii jana, ulieleza kwamba atawaandikia barua rasmi kituo hicho cha redio kutekeleza agizo hilo.
Wasifu wa Ngwea
Jina lake halisi: Albert Keneth Mangwair
Mkoa anaotoka: Ruvuma
Kabila: Mngoni
Kuzaliwa: Mbeya
Tarehe: Novemba 16, 1982
Kuhusu familia: Ni mtoto wa mwisho kati ya 10
Elimu
Shule ya Msingi Bungo: Darasa kwanza mpaka la tano
Mkoa: Morogoro
Shule ya Msingi Mlimwa: La sita mpaka la saba
Mkoa: Dodoma
Shule ya sekondari: Mazengo
Chuo :Chuo cha Ufundi Mazengo





No comments:
Post a Comment