TAASISI
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini mkataba na chuo Kikuu cha
Jagiellonian kilichopo nchini Poland kwa ajili ya kushirikiana katika
kubadilishana ujuzi wa kutoa huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji
wa moyo.
Mkataba
huo ambao utaanza kutumika mapema mwakani ulisainiwa jana jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha
nchini Poland Prof. Bartlomiej Guzik.
Akizungumza
na waandishi wa habari hizi Dkt. Kisenge alisema JKCI imesaini mkataba
na chuo hicho ili kuweka ushirikiano ambao umelenga kuongeza wigo
katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo pamoja na upasuaji wa moyo katika
Taasisi hiyo.
“Tumesaini
makubaliano ambayo yatawawezesha wataalam wetu kwenda nchini Poland kwa
ajili ya kujifunza namna wenzetu wanavyotoa huduma za matibabu ya moyo
lakini wao pia watakuja hapa kwetu kuona na kujifunza jinsi tunavyotoa
huduma za tiba na upasuaji wa moyo”,
“katika
ushirikiano huu pia tumekubaliana wenzetu hawa watatuletea wataalam
ambao watashirikiana nasi katika kuwahudumia wagonjwa kwa kufanya
matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa moyo hasa kuzibua mishipa ya damu
ambayo imeziba, kubadilisha valvu za moyo bila kupasua kifua upasuaji
unaoitwa TAVI procedure ambao kwa hapa nchini kwetu bado haujaanza
kufanyika”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt.
Kisenge alisema JKCI imeongeza wigo wa kuwa na ushirikiano na mashirika
yanayotoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kutoka nchi 18 ikiwemo
nchi hiyo ya Poland ambayo itaanza rasmi kubadilishana ujuzi na
wataalam wa Taasisi hiyo mapema mwakani.
“Tutaendelea
kuongeza ushirikiano huu wa kubadilishana uzoefu na nchi nyingine
ambazo tunaamini zinatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nia
ikiwa ni kuifanya JKCI kutoa matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo
katika Afrika yote”, alisema Dkt. Kisenge
Naye
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian kilichopo nchini Poland
Prof. Bartlomiej Guzik alisema wamevutiwa kufanya kazi na wataalam wa
afya wa JKCI ili kwa pamoja waweze kutoa huduma za kibingwa za matibabu
na upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
“Kujenga
uhusiano baina yetu na JKCI kutasaidia kuboresha huduma za kibingwa za
matibabu na upasuaji wa moyo lakini pia kutaongeza ubobezi kwa wataalam
hawa wa afya”, alisema Prof. Bartlomiej.
No comments:
Post a Comment