KINGATIBA YA MATENDE NA MABUSHA YATARAJIA KUWAFIKIA WAKAZI MILIONI 4 DAR ES SALAAM - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, November 15, 2022

KINGATIBA YA MATENDE NA MABUSHA YATARAJIA KUWAFIKIA WAKAZI MILIONI 4 DAR ES SALAAM

 

Na. Majid Abdulkarim, WAF – Dar es Salaam

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDS) imepanga kutoa Kingatiba kuthibiti Ugonjwa wa matende na mabusha (Ngirimaji) kwa wakazi wapatao 4,449,499 kwa halmashauri za Temeke, Kinondoni na Jiji la Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa leo na Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele mkoa wa Dar es Salaam (RNTDS), Alex Mkamba ambapo amesema katika wakazi hao wanatarajia kufikia mitaa 407 kati ya 535 na kata 70.

Mkamba ameeleza wanatarajia kutoa elimu kwa watu 1,684 walimu wakiwa 330 na watoa dawa 1354 katika halmashauri tatu za mkoa wa Dar es salaa ambazo ni Temeke,Kinondoni na Jiji la Dar es Salaam.

“Kutokana na utafiti ulofanyika hivi karibuni katika kupima maambukizi na vimelea vya ugonjwa wa matende na mabusha kwa watoto wa darasa la kwanza na la pili, katika mkoa wa Dar es salaam wilaya inayoongoza kwa maambukizi ni Kinondoni kata ya Tandale 3.82%, Temeke kata ya Tandika 2.62% na Jangwani 2.6”, amebainisha Mkamba

Mkamba amesema mkoa wamejipanga kutoa elimu ya kutosha kwa kwa wananchi ili kujenga uwezo wa kutambua ugonjwa unavyo ambukizwa na kuchukua tahadhali kwa kufanya usafi wa mazingira na kutumia vizuri neti za kuzuia kuumwa na mbu.

Pia Mkamba amehimiza wananchi matumizi sahihi ya dawa mara kwa mara pale panapobidi kumeza dawa hizo ili kupunguza maambukizi.

Naye Afisa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDS) kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Clara Jones ameeleza ugonjwa wa matende na mabusha ni hali ya kujaa maji sehemu za mwili kama mikono, miguu, matiti na kwenye sehemu za siri kwa wanaume na wanawake.

“Ugonjwa huu unasababishwa na minyoo inayoishi kwenye mfumo wa majidamu inayojulikana kwa jina la kitaalum “Wuchereria bancrofti” unaoenezwa na mbuu wa aina zote”, amesema Dkt. Clara

Kwa upande wake Afisa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDS) kutoka Wizara ya Afya, Oscar Kaitaba amesema wamewajengea uwezo Waandishi wa Habari wa mkoa wa Dar Es Salaam kuhusu ugawaji wa Kingatiba kuthibiti Ugonjwa wa matende na mabusha (Ngirimaji).



No comments:

Post a Comment