Na Fredy Mshiu
Wakazi
wa Wilaya ya Temeke na Kinondoni na maeneo ya katikati ya Jiji wameanza
kunufaika na huduma ya majisafi kutoka katika mradi wa maji Kigamboni
uliozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe Samia Suluhu Hassani.
Mradi
wa maji Kigamboni umesaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma ya
maji katika maeneo hayo katika kipindi cha kiangazi ambapo kupitia mradi
huu wananchi sasa wanapata huduma.
Akizungumzia
hali ya upatikanaji maji katika wilaya ya Temeke, Meneja wa DAWASA
Temeke, ndugu Crossman Makere ameeleza kuwa hali ya huduma kwa sasa
inaridhisha katika maeneo mengi huku huduma ikiendelea kuimarika huku
akiwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu kwani Mamlaka imejipanga
kuhudumia wananchi wote bila upendeleo.
"Tunaishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huduma ya maji kutoka
mradi wa Kigamboni imekuwa suluhisho kwa kiasi kikubwa katika Wilaya
yetu ya Temeke, maeneo yaliyokuwa yakikosa huduma awali kutokana na
ukame wa muda mrefu sasa yanapata huduma na shughuli za uzalishaji na
maendeleo zinatekelezwa kwa kasi."ameeleza ndugu Makere.
Makere
ametoa rai kwa Wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwani watendaji wa
DAWASA wapo kazini usiku na mchana kuhakikisha kila mwananchi anapata
huduma ya majisafi.
Naye,
Ndugu Nora Magege mkazi wa Uhamiaji-Kurasini ameishukuru Serikali
kupitia DAWASA kwa kutatua changamoto ya maji Kwa wakati na sasa
wanapata maji ya uhakika.
"Hapo
awali baada ya upungufu wa maji uliotokana na ukame kuanza tulipata
changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, hata wakati wa mgao
tulikuwa tunapata sana changamoto. Tunasgukuru sasa huduma imeimarika na
sasa tunafurahia tena huduma hii" ameeleza ndugu Magege
Kwa
upande wake Halima Mkwame mkazi wa Tandale kwa Mtogole amesema
kupatikana kwa huduma ya maji katika mtaa wao kumeleta furaha kubwa hasa
kwa wanawake ambao muda mwingi iliwalazimu kwenda mbali kutafuta huduma
hiyo.
Mradi
wa maji Kigamboni umetekelezwa na DAWASA kwa gharama ya zaidi ya Tsh.
Bilioni 23 huku ukihusisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lenye
ukubwa wa lita milioni 15 pamoja na ulazaji wa mabomba makubwa ya
ukubwa tofauti tofauti.
Maeneo
yanayonufaika mpaka sasa kupitia mradi wa maji Kigamboni ni pamoja na
Mivinjeni, Kurasini, Uhamiaji, Kilwa road, Keko, Tandale kwa Tumbo,
Tandale kwa Mtogole, Tandale Muhalitani, Bondeni Hoteli, Magomeni Suna,
Tandale Yemen, Tandale Chama, Uwazani, Upanga, Ilala, Fire, Keko,
Jangwani, Kariakoo, Kisutu na Posta.
No comments:
Post a Comment