Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, ameiagiza Mamlaka ya
Udhibiti Usafiri Ardhini Nchini (LATRA), kupitia Kitengo cha Huduma kwa
Wateja kufanya kazi saa 24 ili kutatua kwa wakati changamoto za
wasafirishaji.
Naibu
Waziri Mwakibete ametoa kauli hiyo jijini Mwanza mara baada kukagua
shughuli za udhibiti usafiri wa ardhini na kubaini uwepo wa changamoto
mbalimbali ikiwemo utoaji wa vibali vya safari na utoaji wa stika.
“Wasafirishaji
hawa ni wafanyabiashara akichelewa masaa mawili au matatu tayari
amepoteza fedha nyingi na hili ninyi ndio mnasababisha kwa kuchelewesha
kuwapa vibali na stika, jipangeni vizuri kuanzia mkoa mpaka makao Makuu
ili malalamiko haya yaishe", amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu
Waziri Mwakibete ameitaka LATRA kukaa na Jeshi la Polisi Nchini ili
kufanya kaguzi za kushtukiza na kupanga mikakati inayotekelezeka
itakayopunguza ajali nchini kwasababu ajali zimeendelea kuongezeka na
kupoteza nguvu kazi ya Taifa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa
upande wake Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Mwanza, Bi. Halima Lutavi,
ameeleza kuwa changamoto ya vibali mfumo unapokuwa na shida LATRA
huwasiliana na Jeshi la Polisi ili kuwaruhusu wasafirishaji kuendelea na
safari ili kutowachelewesha.
Mfawidhi
Halima ameongeza kuwa kwa sasa Mamlaka inaweka mikakati ya kuboresha
usafiri wa pikipiki na bajaji kwa kutengeneza njia maalum ili
kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa usafiri huo katika miji.
Naibu
Waziri Mwakibete yuko Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku mbili kukagua
miradi ya maendeleo na kuangalia utendaji kazi wa taasisi zilizo chini
ya Sekta ya Uchukuzi.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa Malekezo kwa Afisa
Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Mwanza,
Bi. Halima Lutavi, wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo jijini
Mwanza.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Afisa Mfawidhi wa
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Mwanza, Bi. Halima
Lutavi, wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment