* Abainisha uwepo wa mifumo mipya ya kiutumishi na mishahara
WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia
wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa
mwaka 2022/2023 waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa
Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.
“Lengo
la Mheshimiwa Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji,
waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya
bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu
liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo Bungeni leo (Ijumaa, Novemba 11, 2022) wakati akiahirisha
mkutano wa tisa wa Bunge la 12, jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi
Januari 31, mwakani.
Waziri
Mkuu amewashukuru Wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha
utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na mfumo mzima wa
ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa
elimu ya juu nchini.
Amesema
miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa hisia na kupewa uzito mkubwa na
Waheshimiwa Wabunge wakati wa mkutano huo ni hoja ya ugharamiaji,
upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
“Nyote mtakubaliana nami kwamba lengo la mjadala huo, lilikuwa ni
kutafuta suluhu ya suala la wanafunzi takribani 28,000 wenye uhitaji wa
kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 ambao walikuwa
hawajapangiwa mikopo, kutokana na ukomo wa kibajeti,” amesema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hadi sasa taasisi za umma 455
zimeunganishwa na zinatumia mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na
mishahara ili kupunguza muda wa kuchakata malipo ya mishahara kutoka
siku 14 hadi siku moja pamoja na kuwa na taarifa sahihi za watumishi
wanaotarajia kustaafu.
Akizungumzia
utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa umma, Waziri Mkuu amesema
Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha na kuweka mifumo imara ya
usimamizi wa rasilimaliwatu na utendaji kazi wa watumishi wa umma na
taasisi za umma ili kuhakikisha kuwa mifumo iliyopo na inayojengwa
inasaidia kuharakisha utendaji kazi na usimamizi wa watumishi na inakuwa
na taarifa sahihi kwa lengo la kuongeza tija na utoaji wa huduma bora
kwa wananchi.
Amesema
mfumo huo mpya ambao ulianza kutumika rasmi Mei 2021, umeunganishwa na
mfumo wa PSSSF kwa ajili ya kubadilishana taarifa za michango ya
watumishi na nyaraka za hitimisho la ajira; mfumo wa mikopo ya elimu ya
juu (HESLB) kwa ajili ya kubadilishana taarifa za mikopo ya elimu ya juu
kwa watumishi; mfumo wa ajira portal kwa ajili ya kubadilishana taarifa
za waajiriwa wapya na mfumo wa NIDA kwa ajili ya kubadilishana taarifa
za utambulisho wa Taifa wa watumishi.
Ameitaja
mifumo mingine iliyojengwa kwa lengo la kukabiliana na changamoto za
upimaji wa utendaji kazi wa watumishi na mikataba ya utendaji kazi ya
taasisi kuwa ni Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma
(PEPMIS) na Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma
(PIPMIS).
“Ujenzi
wa mifumo hiyo mipya umekamilika. Hivi sasa inafanyiwa majaribio na
inatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa majaribio na kutoa mafunzo
kwa watumishi katika taasisi zote za umma,” amesema.
Amesema
hatua ya mifumo hiyo kuwa ya kielektroniki itaondoa muhali, hisia za
kupendeleana au kuoneana katika usimamizi wa utendaji kazi na
itahamasisha uwajibikaji wa hiari wa watumishi wa umma itakayosaidia
utoaji huduma bora na kwa wakati kwa umma wa Watanzania.
No comments:
Post a Comment