Serikali
imewahakikishia wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga,
Kilimanjaro na Arusha kuwa hakutakuwa na ongezeko la nauli ya treni
inayopita katika mikoa hiyo ili kuwawezesha kufanya safari zao kwa
urahisi hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Akizungumza
jijini Arusha, mara baada ya kutembelea Stesheni ya reli ya kati Naibu
Waziri Mwakibete amesema kuwa uwepo wa treni hiyo umerahisisha shughuli
za usafirishaji wa abiria na mizigo baina ya Dar es Salaam na mikoa hiyo
na hivyo Serikali inatarajia kuongeza idadi ya mabehewa ili kuwawezesha
abiria wengi zaidi kutumia usafiri huo.
“Toka
kuanzishwa kwa safari za treni kwa mikoa hii mwaka 2020 kumekuwa na
ongezeko kubwa la abiria na mizigo na kazi ya Serikali ni kutoa huduma,
hivyo niwahakikishie wananchi kuwa Serikali itaendelea na nauli zile
zile pamoja na ongezeko la abiria ili kuwawezesha kuweza kwenda
kusalimia ndugu zao mwisho wa mwaka’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu
Waziri Mwakibete amesema safari za treni zinatarajiwa kuongezeka kutoka
safari tatu (3) kwa wiki mpaka safari nne (4) kwa wiki mara mabehewa
mapya yatakapowasili mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.
Aidha,
ameongeza kuwa Serikali kupitia Shirika la Reli Nchini (TRC) inaendelea
na ukarabati wa mabehewa takribani 600 lengo likiwa ni kuhakikisha kuna
mabehewa ya kutosha ya kusafirisha abiria na mizigo.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa TRC, Focus Sahani amesema
kwa sasa kupitia treni hiyo wameweza kusafirisha zaidi ya tani 11,600
za mizigo na ambao husafirishwa kwa safari moja ni zaidi ya 300.
Sahani
ameongeza kuwa kuanza kwa treni hiyo kumeleta mafanikio kwani wananchi
wamepata ahueni ya kupungua kwa bei ikiwemo saruji kushuka kutoka
shilingi 20,000/- kwa mfuko mmoja mpaka shilingi 15,000/-
Naibu
Waziri Mwakibete yuko mkoani Arusha kwa ziara ya siku mbili kukagua
miradi ya maendeleo na kuangalia utendaji wa taasisi zilizo chini ya
Sekta ya Uchukuzi.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa Kaimu
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Reli Nchini (TRC) Focus Sahani
(katikati) na Stesheni Masta wa Arusha, Victor Ningo (kulia) wakati
alipotembelea stesheni hiyo jijini Arusha.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akizungumza na abiria wanaotumia
treni ya Dar es Salaam hadi Arusha,wakati alipotembelea stesheni hiyo
jijini humo.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Stesheni Masta wa
Arusha, Victor Ningo, kuhusu utendaji wa kazi stesheni hapo wakati Naibu
Waziri huyo alipotembelea stesheni hiyo jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment