WACHUNGAJI: MAONO YA ALEX MSAMA KUOMBEA UCHAGUZI MKUU 2025 NI YA MUHIMU KWA TAIFA - MAGENDELA BLOG

Recent-Post

ads header

Tuesday, April 15, 2025

WACHUNGAJI: MAONO YA ALEX MSAMA KUOMBEA UCHAGUZI MKUU 2025 NI YA MUHIMU KWA TAIFA

Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), baada ya kufanya kikao na viongozi wa dini, Aprili 12, 2025 Mgahawa wa Food Point jijini Dar es Salaam cha kujadili maandalizi ya uzinduzi wa Tamasha la Kitaifa la kuombea uchaguzi mkuu. Kushoto ni Askofu Ndesario Mlaki kutoka makanisa ya Kipentekosti na kulia ni Mchungaji Mika Fanka wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) la Beroya.

.......................................

NA DOTTO MWAIBALE

WACHUNGAJI wa makanisa ya kiroho Mkoa wa Dar es Salaam wamesema maono ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama ya kufanya matamasha ya kuombea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi oktoba mwaka huu ni ya muhimu kwa Taifa na yatachochoa amani nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, maaskofu, wachungaji na mitume wa makanisa hayo katika kikao cha maandalizi ya tamasha hilo kilichofanyika Mgahawa wa Food Point jijini Dar es Salaam Aprili 12, 2025 kilichoandaliwa na Alex Msama walisema maono hayo ya kimungu yana tija kubwa ni ya mhimu kwa Taifa.

Mchungaji Mika Fanka wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) la Beroya la Kipunguni alisema maono hayo ya Alex Msama na uamuzi wa kuwashirikisha viongozi wa dini kuliombea taifa wakati wa kipindi hiki muhimu cha uchaguzi ni ya kimungu na yanapaswa kuungwa mkono na kila mtu hapa nchini.

“Sisi kama kanisa na wawakilishi wa Mungu moja ya majukumu yetu ni kuliombea taifa na viongozi wetu ili waweze kutuongoza kwa haki na tuwe na amani hivyo maono haya makubwa ya Mkurugenzi Alex Msama kwa taifa letu tunampongeza sana na Mungu akubariki,” alisema Mchungaji, Fanka.

Mchungaji Philipo Mdara wa Kanisa la Free Pentekoste Church Tanzania (FPCT), Gongolamboto Mwisho wa Lami alipongeza hatua hiyo ya Msama ya kuanzisha jambo hilo na kuwaweka pamoja viongozi wa dini ilikufanya maombi ya pamoja.

“Amani ya Taifa lolote inatokana na maombi ya viongozi wa dini hivyo nimpongeze Msama kwa jambo hili hivyo nichukue nafasi hii kuwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi eneo litakalopangwa kufanyika uzinduzi wa maombi hayo ya kitaifa yatakayoanzia jijini Dar es Salaam,” alisema Mchungaji Mdara.

Kwa pande wake Askofu Ndesario Mlaki kutoka makanisa ya Kipentekosti alisema Msama miaka yote amekuwa akiandaa tamasha la Pasaka lakini kutokana na jambo kubwa la kitaifa la  uchaguzi mkuu Mungu alimfunulia maono ya kuja na jambo hilo ili kipindi chote cha uchaguzi nchi iwe na amani na utulivu.

Mchungaji Rose David wa Kanisa la SWS Saa ya Wokovu ni Sasa aliwataka watanzania kushiriki maombi hayo makubwa kama ilivyo kuwa wakati wa Corona hivyo ame waomba wazee, vijana, wakina mama, baba na watoto kwenda kwenye uzinduzi wa maombi hayo ya kitaifa.

Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya kikao na viongozi hao wa dini alisema uzinduzi wa tamasha hilo utafanyika Juni 21, 2025 jijini Dar es Salaam na kuwa wanafanya mchakato wa kuona watafanyia wapi lakini kutokana na umuhimu wake na kuwa ni jambo la kitaifa wanaendelea kuomba lifanyike Uwanja wa Uhuru au wa Benjamin Mkapa kwani bado hawajapata majibu kutokana na viwanja hivyo kuwa katika  ukarabati.

Alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na kuwa siku hiyo ya uzinduzi kutakuwa na wanamuziki kutoka mataifa mbalimbali kama Afrika Kusini, Zambia, Nigeria, Rwanda, Congo, Uganda na Kenya kwa ajili ya kutoa burudani.

“ Mchakato tunaoendelea nao hivi sasa ni pamoja na kumpata mgeni rasmi ambaye atakuwa wa ngazi ya juu pamoja na kuwaomba wadhamini wa kutu sapoti kwani tamasha hili litakuwa na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kuwaleta wanamziki hao ambao watahitaji chakula, malazi, usafiri na kuwalipia wanapoingia nchini,” alisema Msama.


Askofu Ndesario Mlaki kutoka makanisa ya Kipentekosti, akizungumza.
Mchungaji Philipo Mdara wa Kanisa la Free Pentekoste Church Tanzania (FPCT), akizungumza kwenye mkutano huo.  

Mchungaji Mika Fanka wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) la Beroya la Kipunguni, akizungumza.

Mchungaji Rose David wa Kanisa la SWS Saa ya Wokovu ni Sasa, akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Mchungaji, Alex Kishimba, akisisitiza jambo katika mkutano huo.
Viongozi wa dini kutoka makanisa ya kiroho wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao hicho kikiendelea.

 Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama (wa tatu kutoka kulia), akiwa na viongozi wa dini wakati akizungmza na waandishi wa habari.

No comments:

Post a Comment