NA MWANDISHI WETU
TAASISI ya isiyo ya Kiserikali ya Jamii Kwanza initiative (JKI), kwa kushirikiana na Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Amani Kata ya Kipunguni,Ilala Jijini Dar es Salaam, wametoa mkono wa Eid kwa makundi maalum, yakiwemo Yatima na Wajane.
Shughuli hiyo imefanyika jana, Machi 29,2025 lengo likiwa kufanikisha watu wenye uhitaji waweze kusherehekea Sikukuu ya Eid El Fitri kwa utulivu, upendo na furaha.
Akizungumza baada ya kugawa sadaka hiyo Mkurugenzi wa JKI, Daniel Migera amesema kitendo walichokifanya ni moja ya jukumu lao kama taasisi, kurejesha shukrani kwa jamii na kudumisha amani,upendo na furaha.
"Tumeamua kunyoosha mkono ili kudumisha amani na umoja, tumetoa swadaka hiyo ili kuwawezesha na wao kufurahia hii muhimu kwao mara baada ya kumaliza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani " amesema Migera.
Pia Migera ametoa Rai kwa taasisi nyingine wakiwemo wadau mbalimbali, watu wenye uwezo kuwasaidia wenye uhitaji maalum kwani kufanya jambo kama hilo ni muhimu kwa kujenga amani, umoja, mshikamano na furaha kwenye Jamii.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Abdi Hashim Mahanyu ameishukuru JKI kwa kuwaunga mkono na kufanikisha kuwapa mkono wa Eid, Watoto Yatima,Wajane na wenye uhitaji kwa kuwapa chakula ili waweze kufurahia Sikukuu hiyo vizuri.
Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kivule Mashabiki na Mdau wa taasisi hiyo, ameishukuru Serikali ya Mtaa huo kwa kukubali kushirikiana na JKI na kuona umuhimu wa kuwakimbilia wenye uhitaji.
Aidha ameweka wazi kuwa kitendo hicho ni suala la kiimani na katika mafundisho ya dini zote mbili lipo la kuhurumiana na kupendana.
Mmoja ya wakinamama waliopewa sadaka hiyo, Jamila Ally ameishukuru taasisi hiyo pamoja Ofisi ya Serikali ya Mtaa wao kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia na kuweza kuwapa sadaka hizo.
Katika mfungo huu tumeona viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakitoa sadaka kwa makundi ya watu mbalimbali ikiwa ni katika kufanya matendo mema katika mwezi huu, ambapo Waislam na Wakristo wamefunga kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment